Wagombea 13 walikuwa kwenye karatasi ya kura katika uchaguzi wa rais wa 2023 Sierra Leone. / Picha: Reuters

Rais Julius Maada Bio amewataka raia wa Sierra Leone kuwa watulivu wakati shughuli ya kuhesabu kura ikiendelea kufuatia uchaguzi wa Jumamosi.

"Tunaposubiri kutangazwa rasmi kwa matokeo kutoka kwa Tume ya Uchaguzi ya Sierra Leone, ninahimiza kila mtu kuwa mtulivu, kuweka imani katika mifumo na kuendelea kulinda amani na umoja wetu," alisema kwenye Twitter siku ya Jumapili.

Samura Kamara, mmoja wa wagombea 13 katika uchaguzi wa rais, amewataka raia wa Sierra Leone "kuungana na kusonga mbele."

"Shukrani za dhati kwa taifa na kila mpiga kura ambaye alitoa sauti yake [kusikika] katika chaguzi zetu za urais, ubunge na mitaa. Kushiriki kwako ndiko kunakochochea demokrasia yetu,” Kamara alisema kwenye Twitter.

Ushindani wa karibu

Kura za maoni zinatabiri mchuano wa karibu kati ya Rais Bio na Kamara, mgombea wa upinzani.

Takriban watu milioni 3.4 walikuwa wamejiandikisha kuwa wapiga kura kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Juni 24, 2023 wa Sierra Leone.

Upigaji kura kwa kiasi kikubwa ulikuwa wa amani, huku mifuko ya ghasia na madai ya wizi yakiripotiwa katika baadhi ya maeneo ya nchi.

Katika taarifa yake siku ya Jumamosi, tume ya uchaguzi ilisema ghasia zilifanywa dhidi ya wafanyakazi wake wakati wa usafirishaji wa nyenzo za uchaguzi, na kuyataja mashambulio hayo kuwa "bahati mbaya".

"Hii ni hali ya kusikitisha kwa sababu uhamishaji wa nyenzo hizi unafanywa kwa mujibu wa sheria," tume hiyo ilisema.

Zoezi la 'Uwazi'

Kuhusu madai ya ujazo wa kura na aina nyingine za wizi, tume ya uchaguzi ilisema madai hayo si ya kweli kwa sababu "maafisa wa polisi na waangalizi wa uchaguzi walikuwepo katika vituo vyote vya kupigia kura."

Kucheleweshwa kwa kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura kulishuhudiwa katika maeneo ya magharibi mwa nchi na wilaya za mijini, na kusababisha rabsha miongoni mwa wapiga kura. Tume ya uchaguzi ilisema ilipokea nyenzo za kupigia kura kuchelewa, na kusababisha kucheleweshwa.

Baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura saa kumi na moja jioni siku ya Jumamosi, kuhesabu kura kulianza.

Uhesabuji kura, hata hivyo, ulianza saa nane usiku siku ya Jumapili katika vituo vingi nchini, huku zoezi hilo likitarajiwa kuchukua zaidi ya siku moja kukamilika.

Bio, ambaye amekuwa Rais wa Sierra Leone tangu Aprili 2018, anatarajia kumpiku mpinzani wake mkuu Kamara kwenye mechi ya marudiano.

Bio kutoka Chama cha Sierra Leone People's Party (SLPP) alipata kura milioni 1.3 na kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa 2018, huku Kamara wa Chama cha All People's Congress (APC) akiibuka wa pili kwa kura milioni 1.2.

TRT Afrika