Mwanasiasa huyo Ousmane Sonko mwenye umri wa miaka 49 amefungwa jela tangu mwisho wa mwezi Julai / Picha: AFP

Aidha, mmoja wa upande wa Sonko, Bassirou Diomaye Faye naye pia amewasilisha ombi lake la kugombea, kwa mujibu wa Ousseynou Ly, afisa wa chama kilichofutwa alisema Jumanne.

Kama wagombea wengine, Sonko alikuwa na hadi Disemba 26 kuwasilisha nia yake ya kugombea na kuonyesha kuwa amekusanya saini za kutosha.

Wiki iliyopita, taasisi kuu nchini Senegal inayosimamia uchaguzi, ilimnyima mwakilishi wa Sonko nyaraka zinazohitajika kuwasilisha ombi la kugombea urais.

Hata hivyo, hali hiyo haikuwanyima mawakili wa Sonko kuwasilisha ombi lake, huku wakitumaini kwamba mfumo wa haki ungekuwa wenye kukubali zaidi.

"Tuna amini kuwa ugombea wake utakubaliwa na kuthibitishwa," Larifou, mmoja wa mawakili wake, alisema Ijumaa katika kikao na waandishi wa habari mjini Paris.

"Baraza kuu la katiba ni chombo cha uadilifu na si cha kisiasa."

Sonko alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela Juni 1 kwa tuhuma za kuwapotosha watoto. Alikataa kuhudhuria kesi yake na akahukumiwa bila kuwepo.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 49 amefungwa jela tangu mwisho wa mwezi Julai kwa tuhuma nyengine ikiwemo uasi, kula njama na makundi ya kigaidi na kuhatarisha usalama wa taifa.

Sonko amekanusha mashtaka yote, akijitetea kuwa yamekusudiwa kumzuia kumpinga Rais Macky Sall katika uchaguzi wa Februari 25.

Katikati ya mwezi huu wa Disemba, hakimu mmoja aliamuru kwamba ajumuishwe tena kwenye orodha ya wagombea, akithibitisha amri ya mahakama ya chini ambayo ilikuwa imepinduliwa katika rufaa ya kwanza.

Faye, ambaye naye pia yuko gerezani, ndiye mgombea mbadala wa Chama cha Pastef, ambacho mamlaka iliamuru kufutwa mnamo Julai.

Waziri mkuu wa zamani Aminata Toure, ambaye wakati mmoja alikuwa mshirika wa Sall lakini tangu wakati huo amejiunga na upinzani, pia alisema Jumatatu alikuwa ameomba kugombea uchaguzi wa rais.

AFP