Kiongozi wa Senegal, Macky Sall anapitia shinikizo kubwa la kupanga tarehe mpya ya uchaguzi. Picha:/ SallX  

Rais wa Senegal Macky Sall amesisitiza kwamba utawala wake utaishia tarehe 2 Aprili, bila kuweka bayana tarehe kamili ya uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo, ambao uliahirishwa mapema mwezi huu.

Kiongozi huyo amekumbana na kelele na malalamiko ya kutangaza tarehe ya kufanya zoezi hilo, baada ya uamuzi wake wa ghafla wa kuchelewesha uchaguzi wa February 25, na kusababisha hali ya 'sintofahamu' nchini humo.

Sall aliamua kuahirisha uchaguzi huo baada ya mivutano ya kisiasa na kijamii, akisubiria majadiliano ya kisiasa yatakayoanza Jumatatu.

Siku ya Alhamisi, Sall alitangaza mpango wake wa kuwaachia wafungwa wa kisiasa wawili Ousmane Sonko na Bassirou Diomaye Faye, katika namna yake ya kuutuliza umma wa Senegal.

Kumalizika kwa muhula wa Sall

"Muhula wangu utamalizika April 2, 2024," alisema Rais huyo, katika hali ya kuondoa uvumi kuwa akiendelea kukaa madarakani kwa muda mrefu zaidi.

"Tunasubiria kuona nini kitaafikiwa kwenye majadiliano hayo," aliongeza Sall, katika mahojiano ya moja kwa moja ya Televisheni.

"Uchaguzi unaweza kufanyika kabla au baada ya tarehe 2 Aprili," alisema.

Lakini alipobanwa zaidi na maswali, Sall aliweka wazi kuwa isingekuwa rahisi kwa zoezi hilo kufanyika kabla ya Aprili 2.

Sall alisema kuwa atafanya mazungumzo na wagombea Urais siku ya Jumatatu na Jumanne na wadau wengine wa vyama vya siasa nchini humo.

Machafuko ya Senegal

"Lazima tuwe na tarehe ya uchaguzi baada ya mazungumzo hayo," alisema.

Sall alitangaza kucheleweshwa kwa siku ya uchaguzi saa chache kabla ya kuanza kwa kampeni. Uamuzi huo uliungwa mkono na Bunge, pamoja na kuwepo na upinzani mkali, ambapo Sall aliamua tena kutenga mwezi wa Disemba kama tarehe ya uchaguzi.

Upande wa upinzani ulilaani maamuzi ya Sall, na kudai kuwa chama chake kilihofia kupoteza uchaguzi huo, linaripoti shirika la habari la AFP.

Ucheleweshwaji huo uliibua vurugu katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi na kusababisha vifo vya watu wanne.

Viongozi wa Upinzani

Vurugu zimezuka tangu Rais Macky ahairishe uchaguzi wa Rais.Picha: AFP

Wiki iliyopita, taasisi ya katiba ya nchi hiyo ilipinga ucheleweshwaji huo and kutoa wito wa kufanyika kwa uchaguzi haraka iwezekanavyo.

Rais Sall, aliliambia baraza lake la Mawaziri kuwa tarehe ya uchaguzi itapangwa ndani ya muda mfupi.

Kiongozi huyo alisema kuwa anafikiria kuwasamehe wapinzani wake wa kisiasa, kupitia mahojiano aliyofanya siku ya Alhamisi.

Alisema kuwa alitaka kumwachia huru kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko, ambaye amekuwa kifungoni toka Julai mwaka jana, kwa tuhuma za uasi.

"Niko tayari kufanya hivyo ili kila mtu anufaike na msamaha ili amani itawale wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi," alisema Sall.

Mkutano wa Hadhara

Sonko ana ufuasi mkubwa kupitia misimamo yake ya Kiafrika dhidi ya ukoloni wa Kifaransa.

Akimzungumzia kiongozi wa upinzani Bassirou Diomaye Faye, ambaye pamoja na kuwa kifungoni, atagombea urais, Sall alisema kuwa "kabla ya kupitishwa kwa sheria hizo, Faye ataachiwa huru kwa muda, ili kuitikia wito wa mazungumzo".

Awali, Sall alinukuliwa akisema kuwa alitamani sana uwepo wa mazungumzo, ili kupunguza mivutano na kuiomba wizara ya sheria kumalizia uandaaji wa sheria ya itakayotumika katika upatanisho.

Mamia ya wanachama wa asasi za kiraia na kutoka vyama vya kisiasa, waliachiwa huru wiki iliyopita.

'Uchelewaji'

Hata hivyo, vikundi vya asasi za kiraia wametoa wito wa kufanyika kwa mkutano mwingine wa hadhara siku ya Jumamosi, mjini Dakar, ili kuweka shinikizo, baada ya kukusanya maelfu ya watu wikiendi iliyopita.

Siku ya Jumatano, Faye alimtuhumu Sall kwa kuendelea kuchelewesha tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi.

Lawama hizo, pia zilitolewa na watia nia wengine na kumtuhumu Sall kwa kuwa na "nia ovu".

Kupitia taarifa, Faye alisema kuwa atakuwa tayari kwa mazungumzo ya kupanga tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi, bila ucheleweshwaji mwingine na kabla ya kumalizika kwa muhula wa utawala wa Sall.

Sall, ambaye amekuwepo madarakani toka mwaka 2012, alisema kuwa ilimbidi kuahirisha uchaguzi huo kufuatia mizozo kuhusu kutokidhi kwa vigezo vya wagombea na hofu ya kurejea kwa machafuko yaliyoonekana mnamo 2021 na mwaka jana.

Sall ameweka wazi kuwa hana nia ya kusalia madarakani na kugombea kwa mara ya tatu, pamoja na uwepo wa tuhuma hizo kutoka upinzani.

TRT Afrika