Na Ferhat Polat
Februari 17, 2024, nchi ya Libya ilitimiza miaka 13 kamili toka yalipotokea mapinduzi makubwa ya kisiasa, hata hivyo bado raia ya nchi hiyo hawana furaha kutokana na kuongezeka kwa machafuko ya kisiasa nchini humo.
Toka Muammar Gaddafi aondolewe madarakani mwaka 2011, nchi hiyo imetumbukia kwenye vurugu za kisiasa. Jaribio la kupindua utawala wa Gaddafi haukufanikiwa kuanzisha mifumo imara ya kisiasa. Kwa awamu nyingi sasa, Libya imeendelea kujikuta katika machafuko ya kisiasa.
Toka mwaka 2014, nchi hiyo imeshuhudia mpasuko mkubwa kati ya tawala zinazohasimiana, hali iliyosababisha kuibuka kwa vikundi vingi vya wanamgambo. Hatimaye, Libya iliingia kwenye mzozo kutokana na kuchochea uhasama kati ya vikosi vya kisiasa na kijeshi.
Kati ya 2014 na 2021, nchi hiyo kutoka Afrika Magharibi iligawanyika katika pande mbili zinazohasimiana, moja ikiwa Tripoli na nyingine ikiwepo Tobruk.
Ilipofika Machi 2021, serikali mpya ya mpito, iliyojulikana kama serikali ya umoja wa kitaifa ilianzishwa. Serikali hiyo ilichaguliwa kupitia mchakato uliongwa mkono na Umoja wa Mataifa na kuidhinishwa na bunge la mrengo wa Mashariki.
Uidhinishaji huu ulikuwa hatua muhimu kwa Libya, kwani uliashiria kuanzishwa kwa serikali ya umoja kwa mara ya kwanza tangu 2014. Kuanzishwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa ulileta utulivu wa kisiasa na matarajio ya kufanya uchaguzi wa wabunge na urais mnamo Desemba 2021.
Hata hivyo, mpango huo haukutimia kama ilivyotarajiwa na kupelekea kuahirishwa kwa uchaguzi.
Ukosefu wa Usalama
Katika miaka 13 iliyopita, hali ya usalama nchini Libya imekuwa ni kizungumkuti kwa sababu pande zinazohasimiana kushindwa kufikia muafaka. Hali hiyo imesababisha ombwe kubwa la usalama ndani ya nchi hiyo.
Vitisho vya kiusalama vimetoka kwa vikundi vya wanamgambo kutoka Magharibi na Mashariki mwa Libya.
Hii ilitokana na sababu kuwa Khalifa Haftar, ambaye aliongoza kikosi cha Jeshi la Kitaifa la Libya (LNA), inayojumuisha wanamgambo na vikundi vya mamluki.
Ombwe hili lilisababisha mamluki kutoka nje ya nchi kama kile cha Urusi cha Wagner kutumia fursa hiyo kukita mizizi nchini humo, na kudhibiti visima vya mafuta vya Libya.
Mgawanyiko huu, katika ngazi ya kisiasa na usalama, umepelekea ushindani mkubwa wa rasilimali ya mafuta. Hali hiyo ilipelekea bandari na visima vya mafuta kushikiliwa na nchi za kigeni.
Ilipofika Juni 2020, wapiganaji wenye uhusiano na Wagner walidhibiti vituo vikubwa viwili vya mafuta nchini humo, vya El Sharara, na bandari yake.
Libya inajulikana sana kwa kuwa na akiba ya pili kwa ukubwa barani Afrika na inachukuliwa kuwa moja ya nchi tajiri zaidi kiuchumi kulingana na akiba yake kwa kila kichwa.
Kwa bahati mbaya, kutokana na migogoro ya muda mrefu na ukosefu wa utulivu, Libya imekuwa nchi yenye mapato hafifu. Hii imesababisha kuzorota kwa hali ya kijamii na kiuchumi nchini humo.
Mapungufu katika Taasisi
Ujenzi wa serikali umekuwa suluhisho muhimu kwa mahitaji dhaifu na baada ya vita, na husaidia maendeleo ya nchi kuelekea utulivu wa kiuchumi na kisiasa na demokrasia.
Katika hili, vikwazo vikuu vya Libya katika mchakato wa ujenzi wa serikali ni uwepo wa waharibifu na makundi yanayouona mchakato wa amani kuwa ni hatari kwa maslahi na mamlaka yao na kufanya kazi ya kudhoofisha juhudi zozote za ujenzi wa serikali na mchakato wa amani.
Kwahiyo, miaka kumi na tatu baada ya mgogoro wa Libya, jukumu muhimu la kurejesha utulivu katika nchi hiyo liko kwenye umoja wa taasisi za serikali, hususani zile zinazoshughulikia usalama na uchumi.
Ufanisi wa juhudi za kukabiliana na dharura na uokoaji unatiwa dosari na kukosekana kwa mamlaka kuu na uwepo wa vikundi vyenye silaha.
Hii inaongeza changamoto kwenye kuratibu na kutekeleza hatua madhubuti. Zaidi ya hayo, mzozo unaoendelea kati ya vikundi tofauti huzuia ugawaji wa rasilimali na kupunguza kasi ya mchakato wa kujenga upya miundombinu muhimu.
Kwa mfano, kuporomoka kwa mabwawa mawili katika mji wa bandari wa Derna, umesababisha mafuriko makubwa yaliyosababisha vifo, kupoteza makazi na kuharibu mitaa.
Chaguzi zinazosubiriwa kwa hamu
Uchaguzi wa Rais na wabunge uliokuwa ukitarajiwa nchini Libya, ambao ulipangwa kufanyika mwezi Disemba 2021, umeahirishwa kwa muda usiojulikana kutokana na kutokuwepo kwa maandalizi na sintofahamu zinazoendelea miongoni mwa vikosi mbalimbali vya kisiasa kuhusu mfumo wa kisheria wa uchaguzi huo.
Jumuiya ya Kimataifa inatambua kuwa uchaguzi wa Libya ni hatua muhimu katika kushughulikia matatizo na kurejesha uhalali na kujenga mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo.
Kuendesha mchakato wa uchaguzi huru na wa haki kutasuluhisha suala hili kikamilifu. Walakini, uchaguzi ujao katika hatua hii unakabiliwa na changamoto kadhaa. Moja ya mambo makuu ni kukosekana kwa makubaliano ya katiba.
Zaidi ya hayo, pande hasimu za Haftar na Seif al Islam al Gaddafi zinawanawania kiti cha urais, na hivyo kuchangia zaidi mkanganyiko na machafuko katika mchakato huo.
Ili kuanzisha mfumo wa kisiasa wenye ufanisi zaidi, ni muhimu kwenda zaidi ya miundombinu ya sasa. Lengo moja kuu la uchaguzi ni kutoa dira ya taifa, kubainisha sera na mipango ya siku zijazo.
Chaguzi za awali zimekosa ilani na sera za wazi , huku Azimio la Katiba la 2012 likiwa ni dalili ya mwisho ya dira ya kisiasa. Kwa hivyo, kufanya uchaguzi mpya kungewezesha kuundwa kwa mamlaka kwa serikali iliyochaguliwa, kutengeneza njia iliyo mbele.
Ni muhimu kuona namna Uturuki na Misri zilizofanya jitihada kurekebisha uhusiano huo ulioingia dosari, hususani baada ya kuanza kwa mwaka 2021.
Nchi zote, zina uwezo wa kurejesha utulivu nchini Libya, kwa kuzingatia ushawishi wao juu ya pande zinazozozana.
Ankara imeunga mkono Serikali zinazotambuliwa na Umoja wa Mataifa mjini Tripoli, huku Cairo ikiunga mkono LNA ya Haftar. Hata hivyo, licha ya utiifu wao tofauti, mataifa yote mawili yanakubali umuhimu wa kuanzisha upya mchakato wa kisiasa na kutoa uungaji mkono kwa uchaguzi wa kidemokrasia.
Mustakabali wa Libya bado haujulikani kwani inapitia kipindi kigumu cha mpito. Ramani iliyo wazi na ya kisayansi ya kuanzisha demokrasia inahitajika haraka.
Dira hiyo lazima ijumuishe maendeleo ya katiba mpya, kufanya uchaguzi na kuunganisha taasisi za serikali, ambayo itasababisha malengo ya muda mrefu zaidi ya kujenga jamii ya kidemokrasia imara, salama, yenye ufanisi na endelevu nchini Libya.