Makazi ya Waziri Mkuu wa Libya Abdulhamid Dbeibah yalishambuliwa kwa maguruneti / Picha: AFP

Makazi ya Waziri Mkuu wa Libya Abdulhamid Dbeibah yalishambuliwa kwa maguruneti ya kurushwa kwa roketi, ila shambulio hilo halikusababisha majeruhi, waziri wa Libya ameliambia shirika la habari la Reuters.

Waziri huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, alithibitisha katika ujumbe wake siku ya Jumapili kwamba shambulio hilo lilisababisha uharibifu fulani tu. Waziri hajatoa maelezo zaidi.

Raia wawili walisema wamesikia milipuko mikubwa karibu na bahari katika kitongoji cha Hay Andalus huko Tripoli, eneo la makazi ya Waziri Mkuu Dbeibah.

Mwananchi mmoja alisema kuwa baada ya milipuko hiyo mikubwa kusikika, vikosi vikali vya usalama vikiwa na magari yao vilisambazwa kuzunguka eneo hilo.

Mkwamo wa kisiasa Libya imekuwa na amani au utulivu mdogo tangu uasi wa 2011, ulioungwa mkono na NATO, na iligawanyika mnamo 2014, kati ya pande za mashariki na magharibi, na tawala hasimu zikitawala kila eneo.

Serikali ya Dbeibah ya Umoja wa Taifa iliteuliwa kupitia mchakato ulioungwa mkono na Umoja wa Mataifa mwaka 2021, lakini bunge la mashariki mwa nchi, liliacha kutambua uhalali wake mwishoni mwa mwaka huo baada ya kushindwa kwa jaribio la kuandaa uchaguzi wa kitaifa, ambao ulisababisha mkwamo wa muda mrefu wa kisiasa.

Mapema mwezi Machi, viongozi watatu wakuu walisema walikubaliana juu ya "umuhimu" wa kuunda serikali mpya ya umoja ambayo itasimamia uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu.

Dbeibah ameapa kutokabidhi mamlaka kwa serikali mpya bila uchaguzi wa kitaifa.

TRT Afrika