Maandamano nchini kenya yamepinga muswada wa fedha 2024 / Picha: Reuters / Photo: AFP

Jumuia ya Kimataifa imeonyesha kufurahiswa na hatua iliyochukuliwa na Rais wa Kenya William Ruto ya kutosaini Muswada 'tata' wa Fedha wa 2024.

Punde tu, baada ya Rais Ruto kuhutubia taifa, na kuonyesha msimamo wake wa kuutupilia mbali muswada huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony J. Blinken aliongea kwa njia ya simu wa Rais Ruto na kusifu hatua hiyo.

“Waziri amemshukuru Rais Ruto kwa kuchukua hatua za kupunguza hali ya wasiwasi na kusema atawashirikisha katika mazungumzo waandamanaji na asasi za kiraia,” imesema taarifa iliyotolewa na msemaji wa Wizara hiyo Mathew Miller.

Taarifa yake pia imeongeza kusema kuwa, Waziri Blinken ametilia mkazo umuhimu wa vikosi vya usalama katika kuonyesha uvumilivu na kujivuia na vurugu huku akihimiza uchunguzi wa mara moja kuhusu tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu.

Licha ya hatua hiyo ya serikali kutupilia mbali Muswada huo, bado kuna baadhi ya wananachi ambao wanaonekana kutoridhishwa / picha: AFP

Kwa upande wake, kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine amekisifu kizazi cha Gen Z kwa kupaza sauti na hatimae kusababisha Rais Ruto kuufutilia mbali Muswada huo wa Fedha wa mwaka 2024.

Katika ukurasa wake wa X, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield amesema katiba ya Kenya inawahakikishia Wakenya haki ya kuandamana kwa amani.

"Katika siku za hivi karibuni, waliokuwa wakiandamana kwa amani wamekabiliwa na vurugu na risasi za moto. Hakuna Mkenya anatakiwa kudhuriwa wakati akitumia haki yake ya msingi ya mkusanyiko wa amani," asema Balozi Linda.

Hata hivyo, licha ya hatua hiyo ya serikali kutupilia mbali Muswada huo, bado kuna baadhi ya wananachi ambao wanaonekana kutoridhishwa na hatua hiyo huku wakitaka kuwepo kwa maandamano makubwa zaidi yatakayomshinikiza rais wa nchi hiyo kung'oka madarakani.

Kizungumkuti tafsiri ya katiba nchini Kenya

Rais wa nchi hio William Ruto amekiri kushindwa na kusema hadharani kuwa amekataa kutia saini mswada huo. Na badala yake kusema watabana matumizi ya kifedha ili kufikia malengo ya bajeti.

Rais wa nchi hio William Ruto amekiri kushindwa na kusema hadharani kuwa amekataa kutia saini mswada huo/ Picha Kutoka Ikulu Kenya 

Lakini hatua hio ya Ruto ilizua mjadala wa kisheria nchini humo. Nini kinafwata baada ya Raisi kukataa kutia saini mswada wa fedha? Je Rais ana mamlaka ya kuondoa mswada huo ambao tayari umepitishwa na bunge?

Kulingana na katiba ya Kenya, Rais anapaswa baada ya kupokea mswada kutoka bunge ima aidhinishe iwe sharia au kurudisha mswada huo bungeni ufanywe marekebisho.

Asipofanya hivyo mswada huo utapita kuwa sheria baada ya siku 14.

Na upande wao Bunge, baada ya kuzingatia kutoridhishwa kwa Rais, linaweza kupitisha mswada huo kwa mara ya pili, kulingana na marekebisho ya Rais, na hivyo Spika wa bunge anapaswa kurudisha mswada huo kwa rais ili auidhinishe.

Hata hivyo ikiwa bunge halikufanya marekebisho mswada huo kulingana na mapendekezo ya Rais au kufanya marekebisho ambayo hayakubaliani kikamilifu na matakwa ya rais, basi bunge hilo litalazimika kupata theluthi mbili ya kura ya wabunge.

Na iwapo muswada huo utapitishwa utapaswa kurudi tena kwa rais kuidhinishwa kwa muda usio zidi siku saba. Na rais kadhalika atalizimika kuukata au kuidhinisha kwa muda usio zidi siku saba.

Wa ila mswada huo utapita. Lakini bunge lipo mapumzikoni hadi tarehe 22 July, je litaitwa kwenye kikao rasmi cha kupiga kura?

TRT Afrika