Rais wa Kenya William Ruto ameagiza wizara ya leba nchini humo kuongeza mishahara ya kima cha chini zaidi kwa asili mia sita.
Ruto alisema kuwa analenga kuona kila mfanyakazi nchini anafidiwa kulingana na mchango wake katika uchumi wa nchi.
''Nakata kumuagiza waziri wa leba, aite kamati inayohusika na waketi chini, ili kima cha chini zaidi cha mishahara kiongezwe kwa angalau asili mia sita, kisha mniambie vila hesabu hiyo inafanyika,'' alisema Rais Ruto alipohutubia taifa wakati wa sherehe za Leba Dei jijini Nairobi.
''Tunapoadhimisha siku ya Wafanyakazi, tujitolee tena kufanya tuwezavyo na kuchangia tuwezavyo kuboresha ustawi wa kila Mkenya,'' aliongeza Rais Ruto.
Hesabu ya nyongeza ya kima cha chini cha mshahara unahusisha mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na viwango vya mfumuko wa bei, marekebisho ya gharama ya maisha, na viashirio vya ukuaji wa uchumi.
Malalamiko ya watumishi wa umma
Kwa kawaida, serikali hushauriana na vyama vya wafanyakazi, vyama vya waajiri, na wataalamu wa masuala ya kiuchumi ili kubaini kima cha chini cha haki na endelevu.
Kenya imekumbwa na misukosuko ya vyama vya wafanyakazi nchini huku maandamano yakifanyika yanayodai nyongeza ya mishahara.
Muungano mbali mbali za wafanyakazi wakiwemo madaktari na walimu nchini Kenya wamekuwa wakilalamikia mishahara duni na ukosefu wa maslahi ya ustawi kwa wafanyakazi wao huku wakiitisha maandamano ya kususia kazi na kudumaza shughuli katika idara za umma.
Mgomo wa madaktari umeingia siku ya 48 huku kukikosekana matumaini yoyote ya upatanishi au suluhu kati yao na serikali.
Vyama vya wafanyikazi wa sekta ya utumishi wa umma vimeelezea kuunga mkono mgomo wa Wafamasia na Madaktari wa Kenya na Muungano wa Madaktari wa Meno na Maafisa wa Kliniki.
Wajibu wa kutoa Ushuru
Vyama hivyo vimekashifu pendekezo la matamshi ya Waziri wa Utumishi wa umma Moses Kuria ya kubadilisha mikataba ya wafanyakazi wa kudumu kuwa kandarasi za muda kama ukiukaji wa sheria za wafanyakazi wakisema watapinga hatua hiyo kwa gharama yoyote.
Rais William Ruto pia alitoa wito kwa wananchi kujitolea katika kuchangia uchumi wa nchi na kulipa ushuru kama inavyotakiwa.
''Nataka niwakumbushe kuwa nchi hii haiwezi kujengwa kimiujiza,'' alisema Rais Ruto. ''Wenye kujenga Kenya ni sisi sio watu wengine. Nguvu yetu, akili tuliyo nayo, mipango tuliyo nayo na pesa zetu. Na hiyo pesa inatoka kwa ushuru,'' aliongezea katika hotuba yake.
Siku ya Wafanyakazi Duniani, pia inajulikana kama Leba Dei katika baadhi ya nchi au Mei Dei, ni sherehe ya wafanyakazi ambayo inakuzwa na harakati ya kimataifa ya kazi na hutokea kila mwaka tarehe 1 Mei, au Jumatatu ya kwanza katika baadhi ya nchi.
Shirika la Kimataifa la wafanyakazi (ILO) limechapisha taarifa katika mtandao wake kusema kuwa mwaka huu hasa wafanyakazi wanatishiwa na mabadiliko ya tabia nchi na ukuaji wa kasi wa teknolojia.
''Mwaka huu, maadhimisho yetu ya Siku ya Wafanyakazi yana hisia ya dharura ya kujitolea upya kwa haki ya kijamii, tunapopitia magumu ya wakati wetu, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa na mabadiliko ya haraka ya mahali pa kazi kutokana na maendeleo ya teknolojia,'' ilisema taarifa hiyo.
Leba Dei inaadhimishwa kote duniani huku serikali nyingi zikitumia fursa hii kutangaza mageuzi makubwa katika mfumo wa utumishi wa umma na uratibu wa mishahara ya wafanyakazi wake.