Raia wa Mali wamepiga kura siku ya Jumapili iwapo wataunga mkono katiba mpya katika jaribio la kwanza la uchaguzi kwa chama tawala.
Taifa hilo la Afrika Magharibi limekuwa chini ya utawala wa kijeshi tangu mapinduzi ya Agosti 2020 lakini kiongozi wa kijeshi Kanali Assimi Goita, 40, ameapa kuirejesha nchi hiyo kwenye utawala wa kiraia mwaka 2024.
Mali ina wakazi wapatao milioni 21 huku raia wapatao milioni 8.4 wakistahili kupiga kura ya maoni kuhusu maandishi ya katiba mpya. Kura hiyo ya maoni imechochea uvumi kuwa huenda Goita atawania uchaguzi.
Lakini waliojitokeza kwa ujumla walikuwa wachache na ukosefu wa usalama umezuia upigaji kura katika baadhi ya maeneo katika mikoa ya kati na kaskazini ikiwa ni pamoja na mji wa Kidal, ngome ya waasi wa zamani.
Katika Menaka, eneo la kaskazini, upigaji kura ulikuwa mdogo katika mji mkuu wake kutokana na ukosefu wa usalama, maafisa waliochaguliwa wa eneo hilo walisema.
Licha ya wasiwasi huo, hakuna tukio kubwa lililoripotiwa. Upigaji kura kwa ujumla ulikuwa wa amani, Mohammed, mkazi wa mji mkuu Bamako aliiambia TRT Afrika.
Mali mpya
Watu walianza kujitokeza ''polepole'' asubuhi ili kupiga kura zao na baadaye kura zilifungwa saa kumi na mbili jioni kwa saa za huko, Mohammed anasema. ''Waliojitokeza walikuwa wachache sana. Kuna kutojali kutokana na matatizo fulani,'' anaongeza.
Kiongozi wa muda wa Mali Assimi Goita alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kupiga kura, huku wapiga kura wakimiminika katika vituo vya kupigia kura katika mji mkuu, Bamako, mwandishi wa habari wa shirika la AFP alishuhudia.
"Leo ni siku ya kihistoria. Kura hii itabadilisha mambo mengi... Ndiyo maana nilipiga kura,'' alisema mtumishi wa umma Boulan Barro ambaye anaunga mkono mageuzi ya katiba kwa sababu yatatoa ''Mali mpya.''
Timu ya waangalizi kutoka mashirika ya kiraia yanayoungwa mkono na Umoja wa Ulaya waliripoti kuwa kulikuwa na idadi ndogo tu ya masuala ya upigaji kura katika vituo walivyotumwa.
Masuala muhimu
Matokeo ya muda yanatarajiwa ndani ya saa 72 baada ya kupiga kura. Uchaguzi wa urais umepangwa kufanyika Februari 2024.
Rasimu ya katiba hiyo inajumuisha mabadiliko ambayo yamependekezwa katika juhudi zilizopita zilizoshindwa za kurekebisha katiba ambayo wafuasi wanatumai itaimarisha demokrasia na kushughulikia migawanyiko, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa chumba cha pili cha bunge ili kuongeza uwakilishi kutoka kote nchini Mali. Hii ina maana kuwa Mali itakuwa na bunge la chini na seneti.
Pendekezo la kuanzishwa kwa mahakama tofauti ya wakaguzi wa matumizi ya fedha za serikali kutaifanya Mali kuambatana na agizo la Umoja wa Kiuchumi na Fedha wa Afrika Magharibi kutoka mwaka 2000.
Lakini baadhi ya vyama vya upinzani, vikundi vinavyounga mkono demokrasia na wanaharakati wa kura ya 'Hapana' wanasema mamlaka zisizochaguliwa kidemokrasia kama vile utawala wa kijeshi hazina haki ya kusimamia marekebisho hayo makubwa ya katiba.
Pia wanasema katiba inayopendekezwa inakabidhi mamlaka kupita kiasi kwa rais ikiwa ni pamoja na mchakato wa kutunga sheria.
Madaraka ya Rais
"Mimi naunga mkono mabadiliko kwa katiba lakini sio kura hii ya maoni. Uhalali wa wahusika, mchakato ...Nafikiri tungefanya vyema zaidi," wakili Fousseini Ag Yehia alisema katika mji mkuu wa Bamako siku ya Jumamosi.
Junta imetetea kura ya maoni. "Kwa mradi huu, tunaweka imani katika mustakabali wa jimbo letu, kurejeshwa kwa mamlaka yake, na uaminifu mpya kati ya taasisi na raia," rais wa mpito Assimi Goita alisema katika hotuba ya televisheni siku ya Ijumaa.
Katiba mpya itaimarisha nafasi ya rais ambaye atakuwa na haki ya kuajiri na kumfukuza kazi waziri mkuu na wajumbe wa baraza la mawaziri.
Serikali itajibu kwa rais, na sio bunge kama waraka wa sasa wa 1992 unavyosema.
Pia itatoa msamaha kwa waliohusika na mapinduzi ya awali, kurekebisha udhibiti wa fedha za umma na kuwalazimu wabunge na maseneta kutangaza utajiri wao kwa nia ya kubana ufisadi.
Utawala wa kijeshi umetangaza katiba mpya kama suluhisho kwa kushindwa kwa Mali kukabiliana na mizozo mingi.
Matatizo ya hivi majuzi ya Mali yalianza mwaka 2012, wakati waasi wanaotaka kujitenga kaskazini mwa nchi- walioonekana kutengwa na serikali kwa muda mrefu - waliteka maeneo makubwa kabla ya vikosi vya usalama kuwarudisha nyuma. Lakini makundi yenye silaha yanayohusishwa na IS na al Qaeda yaliendelea kufanya mashambulizi.
Uchaguzi wa bunge uliokumbwa na utata wa Machi 2020, na kufuatiwa na maandamano makubwa dhidi ya serikali isiyoweza kudhibiti uasi, ufisadi na mzozo wa kiuchumi, ulimalizika kwa mapinduzi.
Awali Goita alimteua rais wa mpito Bah Ndaw lakini akamtimua katika mapinduzi ya pili mwaka wa 2021 na kuingia kwenye wadhifa wa juu mwenyewe.
Junta ilitoa wito siku ya Ijumaa kuondoka mara moja kwa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo, mhusika mkuu na mwenye utata katika mzozo wa usalama ambao umegharimu maisha ya karibu walinda amani 200 katika muongo mmoja uliopita, shirika la habari la AFP linaripoti.