Umoja wa Mataifa wiki hii imewatunukia medali walinda amani 174 kutoka Rwanda ambao wamekuwa nchini Sudan Kusini chini ya kikosi cha Umoja w Mataifa cha UNMISS.
Medali hiyo iliyopewa jina la ‘UN Service Medal’ yani Medali ya Huduma ya Umoja wa Mataifa ni ya kutambua kujitolea kwa polisi hao katika kuhakikisha amani na usalama nchini Sudan Kusini vinapatikana.
Maafisa waliopewa tuzo hiyo, 160 kati yao ni wa kikosi cha wanawake cha polisi wa Rwanda maafuru (RWAFPU3-5) waliokuwa katika mji mkuu wa Juba, 13 ni maafisa wa polisi (IPOs) na mkuu wa kitengo cha UNMISS, kamishna wa polisi (CP) Felly Bahizi Rutagerura.
Sherehe za utoaji medali zilifanyika katika kambi ya RWAFPU3-5 iliyopo Juba na kusimamiwa na kamishna wa UNMISS Christine Fossen. Shughuli hiyo pia ilihudhuriwa na nchi nyengine zinachangia wanajeshi pamoja na maafisa wa ngazi ya juu wa polisi wa Sudan Kusini (SSNPS).
Kikosi cha RWAFPU3-5 kinahusika na ulinzi wa maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa, watu waliopoteza makazi yao ndani ya nchi na miundombinu muhimu.
Huku majukumu mengine yakiwa ni kuhakikisha usalama, kufanya doria na mengineyo.
Christine ameishukuru serikali ya Rwanda kwa jitihada zake za kuhakikisha nchi hiyo inakuwa miongoni mwa nchi zinazochangia polisi wake.
Amesema: "Ninafuraha kusema kwamba, maamuzi ya Baraza la Umoja wa Mataifa nambari 1325 (2000) yanatilia mkazo jitihada za amani na usalama ambazo ni endelevu pindi wanawake wanapokuwa washirika sawa katika kuepusha migogoro, kupeleka misaada na kutafuta amani ya kudumu.
“Ndio maana imekuwa mafanikio makubwa kwa kikosi cha Rwanda kuwa na uwakilishi wa asilimia 52 ya wanawake."