Polisi nchini DRC wametumia mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya waandamanaji wanaounga mkono upinzani katika mji mkuu wa nchi hiyo Kinshasa ambao wanataka uchaguzi wa urais uliofanyika Disemba 20 kurudiwa.
Wagombea watano ambao ni wapinzani wa rais Felix Tshisekedi wametaka wafuasi wao kufanya maandamano siku ya Jumatano kupinga uchaguzi huo, ambao wanasema haukuwa huru na wa haki, hivyo ufutwe.
Wameahidi kuendelea na maandamano licha ya kupigwa marufuku na serikali Jumanne, kwa madai kwamba, yalikuwa na lengo la kudharau kazi iliyofanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) ambayo matokeo yake mpaka sasa yanaonyesha Tshisekedi akiongoza.
Polisi ilizingira makao makuu ya mmoja wa aliyegombea urais, Martin Fayulu, ambapo waandamanaji walipanga kukusanyika na kuanza maandamano. Baadhi ya polisi hao walikuwa na bunduki na zana za kukabiliana na vurugu.
Hata hivyo, hakukuwa na dalili ya kuwepo kwa mkusanyiko mkubwa kutokana na kutapakaa kwa vikosi vya usalama. Lakini baadhi ya waandamanaji walijaribu kufunga barabara kwa kuchoma matairi, lakini baadae polisi waliingilia kati kwa kutumia vilipuzi vya kutoa machozi. Watu waliokuwa katika makao makuu ya Fayulu waliwarushia mawe polisi.