Wingu la moshi likiwa limetanda kwenye mji wa Khartoum. / Picha: Reuters  

Na

Emmanuel Onyango and Susan Mwongeli

Matumaini ya familia nyingi yanazidi kufifia nchini Sudan, huku nchi hiyo ikiendelea kushuhudia mapigano.

Kulingana na wataalamu, suala la kumaliza mapigano nchini Sudan ni la haraka zaidi.

"Pande zinazohasimiana zimeweka bayana kuwa zitamaliza tofauti zao kwenye uwanja wa vita, jambo ambalo ni gumu zaidi," anasema Tighisti Amare, Kaimu Mkurugenzi wa Mradi wa Afrika katika taasisi ya Chatham House, katika mahojiano yake na TRT Afrika.

"Hali ni mbaya sana, na suala hili halipewi uzito unaostahili," anasema.

Hadi kufikia sasa, hakuna dalili zozote za kumaliza vita vilivyoikumba nchi hiyo toka Aprili 2023.

Tayari, watu zaidi ya milioni 11 wameachwa bila makazi kutokana na vita hivyo, huku wengine milioni 3.1 wakiikimbia nchi hiyo, kulingana Umoja wa Mataifa.

Wanawake wakipita katikati ya majengo yaliyoharbiwa vibaya na vita hivyo.

Kutokuaminiana kati ya viongozi wa pande zinazohasimiana zimezorotesha mazungumzo ya amani na maridhiano, licha ya wito kutoka kwa jumuiya za kimataifa.

Kuongeza shinikizo

"Ni vigumu sana kujua nani watakuwa watu sahihi na nchi sahihi wa kuleta maridhiano. Mpango wa hivi karibuni wa Geneva ulikwama," alisema Amare.

Njia ya kumaliza mgogoro huu bado haijajulikana lakini watalaamu.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, “baadhi ya washirika” wanachochea vita nchini humo.

"Njia pekee ni kuwawekea shinikizo wale ambao wanaendelea kuuzia silaha pande zinazohasimiana," Amare alisema.

"Shinikizo zaidi linahitajika kwa baadhi ya nchi zenye kufanya kazi kwa ukaribu na pande hizo," aliongeza.

Zaidi ya nusu ya watu Sudan wamekosa makazi kutokana na vita hivyo.

Hata hivyo, wataalamu wanasema kuwa vita hivyo havijapewa uzito unaostahili.

Kuzorota kwa hali ya kibinadamu

Machafuko nchini Sudan yamewaweka zaidi ya watu milioni 26 katika baa la njaa, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Licha ya kuwa idadi ya waliopoteza maisha kwenye machafuko hayo inakadiriwa kufikia 27,000 kwa mujibu wa taasisi ya ACLED, wachunguzi wa mambo wanaamini kuwa idadi hiyo inaweza kuwa ya juu zaidi kutokana na hali mbaya ya huduma za afya nchini humo.

Moja ya nchi zinazoongoza jitihada za kupeleka misaada ya kibinadamu nchini Sudan ni pamoja na Uturuki.

‘Amani tu’

"Tunaishukuru sana Uturuki kwa kuwa mstari wa mbele katika kupeleka misaada ya kibinadamu. Zaidi ya meli tatu zimepelekwa ndani ya muda mfupi tu, zikiwa na sheheni ya tani zaidi ya 8,000 ya madawa, malazi na chakula," anasema Nadir Yousif Eltayeb, balozi wa Sudan nchini Uturuki.

Meli ikiwa na shehena ya mzigo wa msaada kutoka Uturuki.

"Lakini nadhani bado kuna pengo kubwa sana kwani zaidi ya watu milioni nane hawana makazi."

Kulingana na mwanadiplomasia huyo, Baraza la Mpito la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdul Fatah al-Burhan, lilikuwa makini kutafuta suluhisho la kudumu.

"Tuko na hamasa kubwa kutafuta suluhu hiyo mapema iwezekanavyo. Hata hivyo, jumuiya ya kimataifa inapaswa kulaani wanamgambo hao," alisema.

Hata hivyo, RSF walisema wako tayari kuwa na mazungumzo na jeshi la Sudan, licha ya kuendelea kwa vurugu zenye kuibua wasiwasi mkubwa wa mustakabali wa wanawake na watoto wa nchini Sudan.

TRT Afrika