Niger imesimamisha matangazo ya BBC kwa muda wa miezi mitatu kutokana na Shirika hilo la utangazaji kutangaza shambulizi la kigaidi mapema wiki hii.
"BBC inatangaza habari za uongo zinazolenga kuharibu utulivu wa kijamii na kudhoofisha ari ya wanajeshi," Waziri wa Mawasiliano Raliou Sidi Mohamed alisema katika barua iliyotumwa kwa redio washirika zinazorusha maudhui ya BBC.
Mohamed alivitaka vituo hivyo kusimamisha vipindi vya BBC "mara moja."
BBC haijatoa taarifa hadharani kuhusu kusimamishwa kazi.
Vipindi vya BBC, ikiwa ni pamoja na vile vya Kihausa, lugha inayozungumzwa zaidi nchini Niger, vinatangazwa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi kupitia washirika wa redio za ndani ili kufikia hadhira kubwa katika eneo lote.
Shirika hilo la BBC liliripoti Jumatano kwamba watu wenye silaha wamewaua zaidi ya wanajeshi 90 wa Niger na zaidi ya raia 40 katika vijiji viwili karibu na mpaka na Burkina Faso.
Niger ilisema ripoti hiyo ilikuwa ya uwongo.
RFI pia imesimamishwa.
Shirika la Utangazaji la Ufaransa la Radio France International pia liliripoti juu ya shambulio hilo lenye idadi sawa ya vifo.
Mamlaka ya Niger ilikanusha kuwa shambulio lilitokea katika eneo hilo katika taarifa iliyosomwa kwenye televisheni ya serikali na kusema kuwa itawasilisha malalamiko dhidi ya RFI kwa "uchochezi wa mauaji ya kimbari."
Niger, pamoja na majirani zake Burkina Faso na Mali, kwa zaidi ya muongo mmoja imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya makundi ya kigaidi, ikiwa ni pamoja na baadhi ya washirika wa al-Qaeda na Daesh.