Wajumbe wa baraza la kijeshi waliofanya mapinduzi nchini Niger wakihudhuria mkutano katika uwanja wa michezo wa Niamey, Niger, Agosti 6. Picha: Reuters

Utawala wa kijeshi wa Niger umefungua tena anga ya nchi hiyo siku ya Jumatatu kwa safari za ndege za kitaifa na kimataifa takriban mwezi mmoja baada ya kufungwa kufuatia hatua ya wanajeshi kumwondoa madarakani rais mteule wa nchi hiyo, vyombo vya habari vya ndani vimesema.

"Uwanja wa ndege wa Niger uko wazi kwa safari zote za ndege za kimataifa na za ndani pamoja na huduma za ardhini bila kikomo," Shirika rasmi la Habari la Niger, Agence Nigérienne de Presse ANP liliripoti, huku likimnukuu msemaji wa Wizara ya Uchukuzi.

Uwanja wa ndege wa Niger Diori Hamani

Hata hivyo, kibali hicho, "hakitumiki kwa safari za ndege za kijeshi na ndege nyingine maalum, ambazo ziko chini ya idhini ya mamlaka husika."

Mamlaka ya kijeshi nchini Niger ilifunga anga ya nchi hiyo mnamo Agosti 6 baada ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) kutishia kuchukua uingiliaji wa kijeshi ili kurejesha utulivu wa kikatiba nchini humo.

Uamuzi huo wa kufunga anga za Niger uliathiri mashirika mengi ya ndege ambayo yanahudumia zaidi Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Taarifa za awali zilionyesha kuwa mashirika mbalimbali ya ndege yalilazimika kugeuka au hata kuahirisha safari za ndege huku zingine zikirekebisha mipango yao ili kutotumia anga kubwa ya Niger iliyoko katikati mwa bara.

Jumuiya ya ECOWAS iliiwekea Niger vikwazo vizito kufuatia kuondolewa madarakani kwa Rais Mohamed Bazoum mnamo Julai 26, ambayo "imeathiri pakubwa" usambazaji wa chakula na vifaa muhimu vya matibabu nchini humo, kulingana na UN.

TRT Afrika