Josephine Mwende anaepiga vita unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu.  Picha: Joséphine

Josephine Mwende Kamene aliyezaliwa na ugonjwa wa kupooza kwa ubongo, hutumia miguu yake kufanya kazi nyingi, na kukiuka changamoto za jamii zinazomkabili, huku akitetea usawa kwa watu wanaoishi na ulemavu.

Josephine Mwende Kamene anapika, anaandika kwenye kompyuta yake na hata kumwandaa mwanawe wa miaka saba kwenda shule kwa kutumia miguu yake – ujuzi aliolazimika kujifunza.

Anaugua kupooza kwa ubongo, hali ya kiafya katika mfumo wa neva inayoathiri harakati za misuli, na namna ya kukaa.

Kutokana na hali hii, sehemu ya juu ya mwili wa Josephine inatetemeka bila kudhibitiwa, na hivyo kufanya iwe vigumu kwake kutumia mikono yake.

"Huenda nisiweze kutumia mikono yangu lakini kwa miguu yangu naweza kufanya mambo mengi kama mtu mwingine yeyote," anaiambia TRT Afrika.

Cerebral palsy affects muscle movement, balance and posture. Photo: Josephine

Ugonjwa wa kupooza kwa ubongo unaweza kutokea ikiwa ubongo wa mtoto haukuwi sawasawa akiwa tumboni, au kuharibika wakati au punde tu baada ya kuzaliwa, wataalamu wanasema.

Josephine alikua hajui kuwa ana ulemavu hadi alipojiunga na shule ya chekechea. Akiwa kwenye uwanja wa michezo siku moja, alitambua kwamba haikuwa rahisi kuzungusha mwili wake kama wanafunzi wenzake.

Tofauti na watoto wengine

"Tulikuwa tukichora kwenye matope na nikagundua kuwa siwezi kunyoosha vidole vyangu kuchora kama watoto wengine," anakumbuka.

"Hapo ndipo nilipogundua kuwa nilikuwa tofauti."

Kulingana na Shirika la Afya Duniani, kupooza kwa ubongo ni mojawapo ya sababu za uharibifu mkubwa wa mwili kwa watoto duniani kote na hutokea kwa angalau watoto wawili kati ya 1,000 wanaozaliwa hai.

Barani Afrika, maambukizi hutofautiana kati ya nchi na kaunti huku inakadiriwa kuwa watoto wawili hadi 10 huzaliwa na ugonjwa wa kupooza kwa ubongo kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai.

Hata hivyo, utafiti unaonyesha kuwa idadi ya kesi barani Afrika inaweza kuwa kubwa zaidi kwani baadhi ya walioathiriwa mara nyingi wananyanyapaliwa na kufichwa mbali na jamii.

Hadithi za uwongo

Ingawa Josephine hakuwahi kufichwa, hata hivyo amekumbana na hadithi nyingi zinazabuniwa kuhusu hali yake.

"Mama yangu aliambiwa mara kadhaa anipeleke kufanyiwa maombi kwa sababu watu wengi walifikiri kuwa nimerogwa," anasema Josephine ambaye alikulia katika kaunti ya Kitui nchini Kenya.

“Hata sasa, nyakati fulani mimi husikia watu wakisema, "Mtazame, anatetemeka. Lazima atakuwa ameshikwa na baridi." Niliwajibu na kuwaambia "Hapana, sijisikii baridi, hii ni hali tu. Hivi ndivyo nilivyo."

Josephine alipokuwa mjamzito mwaka wa 2017, hospitali mbili zilikataa kumlaza kwa ajili ya kujifungua.

"Kwenye hospitali ya pili, muuguzi aliyehudhuria alinitazama na kusema, 'Hatukubali watu kama wewe hapa," anasimulia.

"Nilikuwa na uchungu sana wakati huo kwa sababu maji yangu yashaanza kutoka lakini hakujali. Nilikuwa katika uchungu lakini alikataa kunilaza hospitalini.”

Kunyimwa ajira

Kwa bahati nzuri alilazwa katika hospitali ya tatu aliyoenda na kujifungua mtoto wa kiume mwenye afya njema aliyempa jina la Gift.

Lakini kunyimwa huduma ya afya kwa bahati mbaya haikuwa ubaguzi wake wa kwanza. Pia amenyimwa kazi kwa sababu ya hali yake.

"Niliorodheshwa katika kazi baada ya kukamilisha kwa ufanisi mchakato wa maombi ya mtandaoni kisha nikaalikwa kwenye mahojiano ya kibinafsi," anakumbuka Josephine, mhitimu wa teknolojia ya mawasiliano ya habari.

"Mahojiano yalikwenda kweli lakini nilipowaeleza kuwa ninaandika kwa kutumia miguu yangu, waliniambia kuwa ni kinyume na sera ya kampuni kuweka kompyuta zao za mkononi chini, na hivyo ndivyo nilivyopoteza kazi"

Athari chanya

Alifarijika kujua kwamba mamia ya watu walikuwa wametuma maombi ya kazi hiyo lakini ni wachache tu, pamoja na yeye, walioingia kwenye orodha ya walioitwa kwa mahojiano ya kuandikwa kazi.

"Nimekuwa nikizoezesha akili yangu kuzingatia masuala chanya katika yale ninayoyafanya. Ninaweza kuwa nikitembea barabarani na kumsikia mtu akisema, ‘Loo, yeye ni mrembo sana lakini ana ulemavu. Katika hali kama hiyo najiambia, ‘Angalau wameuona uzuri wangu. Angalau wameona nina akili. Ugonjwa wa kupooza kwa ubongo haunielezi mimi ni nani.”

Mtazamo wake chanya ulimsaidia kuingia katika ulimwengu wa harakati za ulemavu. Anatumia majukwaa yake ya mitandao ya kijamii kukuza ushirikishwaji na kujenga ufahamu kuhusu aina mbalimbali za ulemavu. Pia anajadili baadhi ya masuala ya mwiko yanayoathiri watu wanaoishi na ulemavu.

Kuchupa vikwazo

Josephine ametambuliwa kwa juhudi za kuchupa vizuizi na kubadilisha simulizi juu ya usawa wa kijinsia na ujumuishaji wa kijamii.

“Wazazi wengi wa watoto wenye ulemavu wameniambia kwamba wametiwa moyo na mazungumzo yangu kwenye mitandao ya kijamii. Wananiambia kwamba wanatamani watoto wao wakue na kuwa kama mimi,” asema.

"Hilo linanitia moyo kuendelea kufanya kile ninachofanya, nikijua kuwa ninabadilisha maisha ya mtu kuwa bora na tunaweza kufaulu pamoja.

TRT Afrika