Patricia Kaliati ambaye aliwahi kuwa sehemu ya Baraza la Mawaziri na mbunge nchini Malawi./Picha: Patricia Kaliati  

Mwanasiasa mwandamizi nchini Malawi amepandishwa kizimbani kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo kutishia usalama wa Rais Lazarus Chakwera.

Patricia Kaliati, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama cha United Transformation Movement (UTM), alipandishwa mahakamani siku ya Oktoba 28, mjini Lilongwe nchini Malawi.

UTM ni chama kilichoasisiwa na Makamu wa Rais wa zamani Saulos Chilima, Juni 18 2018, baada ya kuhitalifiana na Rais wa zamani wa nchini Peter Mutharika.

Kaliati alikamatwa siku ya Alhamisi Oktoba 24, akidaiwa kula njama za kumdhuru Rais Lazarus Chakwera.

'Hatua zaidi za kiuchunguzi'

Hata hivyo, mwanasiasa hajazungumza lolote kufuatia tuhuma hizo.

Kwa mujibu wa msemaji wa Jeshi la Polisi la Malawi Peter Kalaya, uchunguzi wa madai hayo uko katika hatua nzuri.

Hata hivyo, Jeshi hilo halikutaka kuweka wazi kiini cha madai hayo, kwa nia ya kuwalinda mashahidi na kutokuharibu uchunguzi wa kesi hiyo.

Inadaiwa kuwa, Kaliati na wenzake wawili walikula njama ya kumdhuru Rais Chakwera, kati ya Mei na Juni mwaka 2024.

Wapewa dhamana

Hata hivyo, siku ya Jumatatu Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini Lilongwe, ilimpa dhamana mwanasiasa huyo.

Mtuhumiwa huyo, alitakiwa atangulize kiasi cha dola 580 kama dhamana.

Aidha, masharti mengine ya dhamana hiyo yanamtaka mwanasiasa huyo kuripoti polisi kila Jumatatu baada, kila baada ya wiki mbili, huku pia akitakiwa awepo muda wote wa kusikilizwa kwa kesi yake.

'Kipindi kigumu'

Mahakama hiyo pia imemkataza kukutana na mashahidi katika kesi hiyo, ikionya kuwa ukiukwaji wowote wa masharti hayo utaondoa haki yake ya kupata dhamana.

Siku ya Jumatatu, Kaliati alichapisha taarifa kwenye ukurasa wake wa Facebook akiwashukuru wanachama wote wa UTM na viongozi kutoka vyama vya upinzani kwa kumuunga mkono wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Chama cha UTM, kupitia msemaji wake Felix Njawala, kinasema kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa Kaliati ni njama ya kisiasa.

Kaliati aliwahi kuwa Waziri wa Jinsia na pia Waziri wa Habari nchini Malawi.

Aliwahi pia kuhudumu kama mbunge wa Mulanje Magharibi nchini humo.

TRT Afrika