Waendesha mashtaka wa Afrika Kusini leo Ijumaa waliongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya mashtaka wanayoleta dhidi ya afisa wa zamani wa polisi wa Rwanda Fulgence Kayishema, ambaye anasakwa kimataifa kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994.
Sasa anakabiliwa na mashtaka 54 tofauti nchini Afrika Kusini yanayohusiana na ulaghai na makosa ya uhamiaji, kutoka matano ya awali, msemaji wa waendesha mashtaka Eric Ntabazalila alisema nje ya mahakama ya Cape Town.
Aliyekuwa afisa wa polisi wa Rwanda mwenye umri wa miaka 62, alikamatwa Jumatano huko Paarl, mji katika Mkoa wa Western Cape nchini Afrika Kusini, baada ya kuwa mafichoni kwa miaka 22.
Anatuhumiwa kwa kuandaa mauaji ya wakimbizi wa Kitutsi takriban 2,000 katika Kanisa Katoliki la Nyange wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Kitutsi nchini Rwanda.
Inakadiriwa kuwa watu 800,000 wa Kitutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa nchini Rwanda mwaka 1994 katika kipindi cha siku 100 cha umwagaji damu.
Kayishema alikamatwa katika operesheni ya pamoja na mamlaka za Afrika Kusini na timu ya kumtafuta wahalifu wa IRMCT (International Residual Mechanism for Criminal Tribunals), kulingana na taarifa iliyotolewa na mahakama maalum ya Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi.
Mwendesha mashtaka mkuu wa IRMCT, Serge Brammertz, alisema Kayishema alikuwa mafichoni kwa zaidi ya miaka 20 na "kukamatwa kwake kunahakikisha kuwa hatimaye atakabiliwa na sheria kwa madai yake ya uhalifu."
IRMCT ilisema mauaji ya kimbari ni uhalifu mbaya zaidi unaojulikana kwa binadamu na jumuiya ya kimataifa imejitolea kuhakikisha kuwa watekelezaji wake watashitakiwa na kupewa adhabu.