Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara ya Afya nchini Tanzania Ntuli Angyelile Kapologwe, ameibuka mshindi wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC).
Dkt. Kapologwe anachukua nafasi hiyo baada ya kuwashinda wagombea wengine sita waliokuwa wakiwania nafasi hiyo katika uchaguzi uliofanyika Februari 12, 2025 nchini Malawi.
Dkt. Kapologwe anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Profesa Yoswa Dambisya wa Uganda ambaye amehudumu kwenye nafasi hiyo kwa mihula miwili ndani ya miaka 10.
Nafasi hiyo ilikuwa ikiwaniwa na jumla ya wagombea 47, huku wagombea saba wakibakia baada ya mchujo.
Mtanzania wa kwanza kushika nafasi hiyo alikuwa ni Dkt. Winnie Mpanju, ambaye alihudumu kutoka mwaka 1993 mpaka 2000.
Ikiwa imeanzishwa mwaka 1974, Jumuiya ya ECSA-HC ina jumla ya nchi wanachama 9.
Nchi hizo ni Tanzania, Malawi, Kenya, Lesotho, Zambia Zimbabwe, Mauritius, Uganda na Eswatini.