Dkt Faustine Ndugulile.Picha:TRT Afrika

Mtanzania Faustine Ndugulile ndiye Mkurugenzi mpya wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kanda ya Afrika.

Dkt Ndugulile aliwashinda Dkt Ibrahima Socé Fall kutoka na Senegal na Dkt Boureima Hama Sambo wa Niger, yeye akiwa amekusanya kura 25, dhidi ya 20 za wawili hao.

Naibu huyo wa Afya wa zamani nchini Tanzania, sasa anachukua nafasi ya Mbotswana Matshidiso Moeti, alihudumu katika nafasi hiyo ya uongozi kutoka mwaka 2015, na kuwa mwanamke wa kwanza kushukilia nafasi hiyo barani Afrika.

Dkt Ndugulile anatarajiwa kuanza rasmi kazi mwezi Februari 2025, ambapo anategemewa kuhudumu nafasi hiyo kwa miaka mitano.

Dkt Ndugulile ni nani?

Akiwa na taaluma ya udaktari, Dkt Ndugulile amebobea katika afya ya umma. Aliwahi kuhudumu kama Naibu Waziri wa Afya nchini Tanzania, kabla ya kuhamishiwa kwenda Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Kwa sasa, Dkt Ndugulile ni makamu mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na pia ni mbunge wa jimbo la Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

TRT Afrika