''Mashambulizi yoyote dhidi ya raia wa Ufaransa au maslahi yake nchini Niger yatachochea jibu kali kutoka Ufaransa,'' serikali ya Ufaransa ilisema Jumapili, wakati maandamano ya wafuasi wa kijeshi yakifanyika nje ya Ubalozi wa Ufaransa huko Niamey kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya wiki iliyopita.
Katika taarifa yake,rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesisitiza kuwa hawezi kuruhusu mashambulio yoyote dhidi ya vikosi vyake, ubalozi au raia wake walioko Niger.
Macron amezungumza na Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum na rais wa zamani wa Niger Mahamadou Issoufou katika saa chache zilizopita, taarifa hiyo ilisema, na kuongeza kuwa wote wawili wamelaani mapinduzi hayo na kutoa wito wa utulivu.
Ufaransa ilitangaza Jumamosi kuwa inakata misaada yote ya maendeleo kwa Niger na kutoa wito wa kurejeshwa kwa Bazoum.