Marais wa Afrika Mashariki wakiwemo Rais wa Rwanda Paul Kagame, William Ruto wa Kenya, Evariste Ndayishimiye wa Burundi, Salva Kiir Sudan Kusini, Samia Suluhu wa Tanzania, Yoweri Museveni wa Uganda na Félix Tshiseked wa DRC. Picha: EAC

Marais wa mataifa ya Afrika Mashariki wakiwemo rais wa Rwanda Paul Kagame, rais wa Kenya William Ruto, rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, rais wa Tanzania Samia Suluhu, rais wa Uganda Yoweri Museveni, na rais wa DRC Félix Tshisekedi watajumuika mjini Arusha, kaskazini mwa Tanzania katika mkutano wa 23 wa wakuu wa nchi EAC.

Katika mkutano huo, rais wa Sudan Kusini Salva Kiir atachukua rasmi uenyekiti wa Jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki kutoka kwa rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye.

Mkutano huo wa siku mbili pia utajadili masuala ya tabia nchi, usalama wa chakula na changmoto mbalimbali za jumuiya huku ukanda ukizidi kukabiliana na matatizo ya amani na usalama wa kikanda, hasa mgogoro wa ndani kwa ndani nchini Sudan na ukosefu wa usalama katika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.

Uenyekiti huo wa EAC ni wadhfa wa mzunguko ambao unashikiliwa na kila nchi mwanachama kwa muhula wa mwaka mmoja.

Vile vile, EAC inatarajiwa kuwasilisha ripoti ya uanacham mpya wa Somalia kwenye mkutano huo wa 23 wa kawaida mjini Arusha.

Somalia ipo katika hatua za mwisho za mchakato wake wa kujiunga na jumuiya ya kikanda ya EAC huku kukiwa na uwezekano wa kukaribishwa rasmi mwishoni mwa mwezi huu katika mkutano wa kawaida wa 23 wa wakuu wa nchi za EAC.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Peter Mathuki amedokeza kuwa Somalia itakaribishwa rasmi kwenye jumuiya hiyo.

Mchakato mzima wa kushirkishwa kwa Somalia uliidhinishwa rasmi kwenye mkutano wa 22 wa kawaida wa wakuu wa nchi za EAC ambao waliielekeza baraza hilo kufuatilia haraka zoezi la uhakiki kwa mujibu wa taratibu za EAC za uandikishaji wa wanachama wapya wa EAC.

TRT Afrika na mashirika ya habari