Na Charles Mgbolu
Ukumbi ulisalia kimya wakati washindi wawili bora wa Miss Afrika Kusini 2023, Natasha Joubert na Bryoni Natalie Govender waliposimama ana kwa ana jukwaani.
Natasha, akiwa amevalia gauni la kujimwaya lililowiva wekundu, hakuweza kumtazama Bryoni, ambaye pia alikuwa akihangaika kujistahi huku uzito wa wakati huo ukiwaingia wote wawili.
Mshindi wa shindano hilo alikuwa karibu kutangazwa, na watazamaji wenye furaha walijawa na jadhba namatarajio.
Hatimaye mtangazaji Bonang Matheba alitangaza matokeo. Ilikuwa Natasha, na machozi ya furaha hayakuweza kuacha kutiririka.
Mshindi wa kwanza alimkumbatia na kumbusu, kisha akarudi nyuma ili kuwika kufanyike.
Malkia anayemaliza muda wake, Ndavi Nokeri, alifanya heshima ya kimila. Nokeri aliweka taji yenye mandhari ya 'Mowana' inayong'aa juu ya kichwa cha Joubert na shada la maua mikononi mwake.
Muziki wa kusisimua uliibuka tena wakati Joubert alipokuwa akitembea na malkia akipunga mkono; alikuwa akicheka na kulia kwa wakati mmoja.
Shindano la Miss Afrika Kusini 2023 lilikuwa na hadhira iliyojaa kwenye Ukumbi wa SunBet katika Time Square mjini Pretoria.
Pia kulikuwa na safu kali ya watumbuizaji wa muziki, wakiwemo Siki Jo-An, Jimmy Nevis, Brenda Mtambo, na Robot Boii, ambao walisisimua watu kwa maonyesho yaliyoandaliwa ya hali ya juu.
Lakini makofi makubwa zaidi yamekwenda kwa mwanamke wa sasa, Natasha Joubert, kwa kupigana vikali ili kupata taji.
''Wakati huu ni kielelezo cha marudio ya matukio kwangu. Ndoto ambayo ilianza miaka 11 iliyopita, "Natasha alisema katika hotuba yake ya kupokea taji.
Natasha, kutoka Tshwane huko Gauteng, ni mhitimu wa shahada ya usimamizi na mauzo na mmiliki na mbunifu wa mitindo wa Natalia Jefferys, kampuni aliyoanzisha alipokuwa na umri wa miaka 19.
Alikuwa mshindi wa pili wa Miss Afrika Kusini 2020 na baadaye aliwakilisha nchi kwenye shindano la Miss Universe 2020 nchini Marekani lakini alishindwa kuingia katika 21 bora.
''Inajihisi kurudi tena na kupewa nafasi ya pili! Najua huu ni ushuhuda ninaohitaji kushiriki na ujumbe wa ajabu: 'Kamwe wewe si zao la hali yako. Wewe ni zao la chaguo lako,' aliambia ukumbi uliojaa baada ya kuingia kwenye orodha ya 12 bora.
Ni dhahiri alikuwa kipenzi cha mashabiki, kwani tangazo lake la ushindi lilipokelewa kwa shangwe nyingi mtandaoni na nje ya mtandao.
‘’Natasha anastahili. Alikuwa mshiriki thabiti zaidi mwaka huu. Alijiandaa kwa wakati huu na alikuwa na nguvu kabisa kuelekea fainali,’’ aliandika shabiki, @wandilemthembu, kwenye Youtube.
''Nataka kukabiliana kikamilifu na changamoto hizi mpya, kukua na kubadilika zaidi kama mwanamke, na wakati huo huo nijiachie na kufurahia kila sekunde,'' Natasha aliongeza.
Anatarajiwa kuwakilisha Afrika Kusini kwenye Miss Supranational 2024.