Na Firmain Eric Mbadinga
Ni furaha kuwatazama jukwaani, namna miguu yao ikifuata midundo na mirindimo ya mifupi mifupi, huku nyuso ziking'aa kwa tabasamu angavu kama mwangaza.
Watoto hawa kutoka Chama cha Watoto wa Kpadomeviwo cha Togo (AKDT) hucheza vizuri chini ya wasanii waliobobea, ushahidi tosha wa ari na uthabiti wao.
Hali ni tofauti wakiwa nje ya jukwaa. Watoto hawa, wenye umri kati ya miaka 6 na 20, hubadilisha sare zao na kurudia mavazi yao ya kawaida ya kila siku na kubakiwa na nyuso zao zenye furaha ambazo huficha taabu zao za kila siku.
Pamoja na kadhia yote wanayopitia watoto hawa, bado wanaweka tumaini lao kwa Koffi Mensah Agbelessessi, ambaye ndiye kiongozi wa kikundi cha ngoma cha AKDT.
Koffi, mwenye miaka 35 alikutana na shida na taabu za watoto hawa baada ya kutembelea kituo cha kulelea yatima huko Atakpamé, mji wa tano kwa ukubwa nchini Togo, alipokuwa ameenda kufanya onesho. Msanii huyo alishtushwa sana na hali aliyokutana nayo pale, hususani kuona hali dhoofu za watoto hawa pamoja na akina mama wanaong’ang’ania mabaki ya mwisho ya mboga mboga.
"Niliona mahitaji ya wale watoto na upendo waliooneshwa na akina mama, ingawa hawakuwa na chochote. Atakpamé ni mji aliozaliwa mama yangu na ndio maana nilihisi muunganiko wa haraka. Nikaamua kuwachukua watoto hao chini ya uangalizi wangu. Ndipo nilipoanza harakati binafsi za kuwasaidia," anaiambia TRT Afrika.
Mwanzo mgumu
Wakati taasisi ya AKDT inataka kuanza mwaka 2017 huko Lomé, Koffi angetembelea fukwe za bahari na mitaani kwa nia ya kuwapa moyo watoto kutokana na changamoto za ugumu wa maisha.
Msanii huyo alitumia mapato kutoka kwenye maonesho yake kuwapangishia watoto hao chumba katika mtaa wa Bè-Ahligo Dekadjev, ili kuwapa hifadhi waliyokuwa wanaihitaji.
Watoto hao walipenda kumwita Koffi “mwalimu”, kama ushuhuda wa imani na heshima yao kwake.
Wakiwa AKDT, watoto hawa kutoka mitaani walijifunza kucheza ngoma ili kujiongezea thamani na kujiamini. Baadhi walipata fursa ya kukutana na kuunganika na familia zao.
Hata hivyo, haikuwa kazi rahisi kwani baadhi ya watoto hawakuwa tayari kuzungumzia usuli wa maisha yao.
Kujengeana imani
Ili kukuza uwazi, Koffi na timu yake huwashirikisha watoto katika mijadala ya mara kwa mara. Wanaume huwashauri wavulana; wanawake wanawashauri wasichana katika mada zisizo na kikomo.
Kila kitu kinajadiliwa kwa uwazi na uaminifu, kutoka masuala ya usafi binafsi, afya, na simulizi za uzoefu wao.
Koffi hutengeneza hereni, shanga za miguuni na mikononi kutoka kwenye plastiki na vitambaa kama msaada wake mwingine kwa chama hicho. Vitu hivyo huuzwa kwenye maonesho ya ndani huko Ulaya, hatua inayokiingizia chama hicho fedha za ziada zitakazosaidia kuwaondoa watoto hao mitaani.
AKDT imeendelea kukua kwa miaka mingi, kama lilivyo wazo la kuunda kikundi cha ngoma na watoto.
Watoto hao walimuomba Koffi awafundishe namna ya kucheza, baada ya kuhamasika na maonesho kutoka kwa “mwalimu” wao.
Koffi aliridhia ombi hilo kwa furaha na kuwanunulia watoto hao madufu, ngoma na sare za kuchezea ili waanzishe kitu kilichokuja kuitwa kikundi cha ngoma cha AKDT.
Zaidi ya ngoma
Mapato yanayopatikana kutoka katika maonesho hutumika kugharamia masomo kwa watoto wenye familia zisizo na uwezo wa kufanya hivyo, au watoto wanaoshindwa kuungana na familia zao.
Ili harakati zake ziungwe mkono na wadau wengine, Koffi amekuwa akitumia njia ya mitandao ya kijamii. Jitihada hizo zimezaa matunda kwani baadhi ya watoto wamefanikiwa kuunganishwa na familia zao, mashirika yasiyo ya kiserikali , wakati wengine bado wako chini ya uangalizi wake, wakiendelea na masomo yao.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya baadhi ya watoto wameamua kurudia maisha ya taabu ya mitaani.
Koffi amesononeshwa sana na hali hii, haswa akitambua adha na mateso ambayo wanakutana nayo watoto hao wakiwa mitaani, kama vile kunyanyaswa na kusafirishwa.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), takriban watoto milioni 30 barani Afrika, huishi mitaani. Kwa nchi ya Togo, yenye watu milioni nane, idadi ya watoto waishio mitaani inafikia 7,000.
Taasisi ya AKDT inatoa afueni kwa watoto hawa, sio tu kupitia sanaa na masomo, lakini kupitia elimu ya ufundi stadi kama vile ususi, upishi na ufundi magari. Haya yote hufanyika kupitia msaada kutoka kwa washirika wenye kuguswa.
Yawezekana safari hii ilikuwa ngumu kwa Koffi, lakini wema na uungwana wa watu, kutoka ndani na nje ya Togo, ambao pia hutoa misaada ya kifedha, vinampa msanii huyo ari ya kuendelea na jitihada zake.
"Pesa hii hutumika kwa ajili ya chakula na huduma za matibabu, kuhakikisha kuwa watoto hawa wanapata mahitaji yao ya kila siku," Koffi anailezea TRT Afrika.
"Baadhi ya watoto hawa wameishia mitaani kutokana na sababu za ukatili na matumizi ya dawa za kulevya ndani ya familia zao, wakati wengine walinyanyaswa. Natumai kuona msaada mwingine ukitolewa kwa watoto hawa."