Kufuatia kufika kwa wagonjwa wa Palestina wa saratani Uturuki,  Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Waziri wa Afya wa Uturuki Fahrettin Koca waliwatembelea. /Picha: AA  

Uchunguzi wa wagonjwa 27 kutoka Gaza ambao waliletwa na Uturuki umethibitika, na matibabu yao yanaendelea, ameandika katika mtandao wa X Waziri wa Afya wa Uturuki Fahrettin Koca.

"Kati ya wagonjwa, 26 wamethibitika kuwa na saratani. Miongoni mwao ni wanawake 12, na wawili wapo chini ya miaka 18. Saratani ya tishu laini imebainika kwa mmoja wa mgonjwa ambae yuko chini ya miaka 18, na mwengine akipatikana na tatizo la damu," amesema Koca.

"Miongoni mwa wagonjwa wetu watu wazima, 8 wameonekana na saratani ya matiti, 4 saratani ya mapafu ikiwa hatua ya 3, 3 wakiwa na tishu laini, 2 saratani ya tumbo, 1 saratani ya nyongo, 1 ya mfuko wa mkojo, 1 saratani ya figo, 1 saratani ya tumbo, 1 saratani ya lymphoma, 1 damu, 1 saratani ya ngozi, na 1 saratani ya ubongo," amefafanua.

Huku uchunguzi na matibabu ya wagonjwa kutoka Gaza ukiendelea katika Hospitali ya Ankara Bilkent City Hospital, amehakikisha kuwa madaktari bingwa wanaendelea na mchakato.

Kuondoka kwao kutoka Gaza iliyozingirwa

Wagonjwa wa saratani na wasindikizaji wao waliondoka kupitia uwanja wa ndege wa kijeshi kaskazini mashariki mwa Misri kuelekea Uturuki kwa ajili ya kupata matibabu.

Fahrettin Koca pia aliwasili katika mji mkuu wa Misri mapema Jumatano na alipokelewa na mwenzake wa Misri Khaled Abdel Ghaffar na maafisa wengine.

Baadae alikwenda katika Hospitali ya Nasr kuwaona waliojeruhiwa kutoka Gaza na kupewa maelezo mafupi kuhusu afya zao.

Alisema, wagonjwa waliopelekwa Uturuki kutoka Gaza ndio Wapalestina wa kwanza kusafiriki kutoka Misri kwenda nchi nyengine kwa ajili ya matibabu.

Akisema kuna takriban wagonjwa 1,000 wa saratani Gaza, amesema wanajaribu kuleta wagonjwa wengi Uturuki kwa kuboresha mawasiliano.

Koca amesema Uturuki imetuma takriban tani 660 za dawa na vifaa tiba, na magari ya wagonjwa 20, pamoja na vituo vya afya 8 vya dharura Gaza katika ndege 10 na meli moja.

TRT World