Kusitisha kwa misaada duniani kutaathiri Sudan ambapo Marekani inachangia asilimia 45 ya misaada kwa watu/ Picha: AFP

Saa chache baada ya kuingia madarakani, Trump aliamuru kusitishwa kwa siku 90 kwa msaada kwa mataifa ya kigeni ili kutathmini kama unakwenda sanjari na vipaumbele vyake vya sera ya kigeni.

Siku ya Ijumaa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitoa amri ya kusitisha shughuli za mashirika mbalimbali ikiwemo ya umma na ya misaada duniani kote yanayotoa usaidizi sasa na ambao umeidhinishwa, ikitilia shaka matumizi ya mabilioni ya dola ya misaada.

" Kila dola tunayotumia, kila programu tunayofadhili, na kila sera tunayofuata lazima tuainishe kwa kujibu maswali matatu rahisi: Je, inaifanya Marekani kuwa salama zaidi? Je, inaifanya Marekani kuwa na nguvu zaidi? Je, inaifanya Marekani kustawi zaidi?” Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisema ,

Marekani ndio mfadhili mkubwa zaidi wa misaada duniani.

Takwimu zinaonyesha Katika mwaka wa fedha wa 2023, ilitoa msaada wa dola bilioni 72. Hii ni asilimia 42 ya misaada yote iliyotumiwa kwa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watu mnamo 2024.

Ujumbe kutoka serikali ya Marekani kwa shirika la USAID ulitishia "hatua za kinidhamu" kwa wafanyakazi wowote wanaopuuza maagizo ya rais.

Fedha kutoka Marekani huchangia pakubwa katika sekta ya afya Uganda/ Picha: Hospitali ya Mulago

Mashirika ya misaada na wafadhili wengine wanahangaika kuelewa jinsi agizo hilo litakavyoathiri shughuli za kuokoa maisha katika mataifa yanayotegemea msaada huo ulimwenguni.

Ni mapema mno kusema kuhusu huduma gani ambazo zitatakiwa kusitishwa, walisema.

Athari kwa Afrika

Takwimu za USAID zinaonyesha nchi 31 barani Afrika zinapata msaada kutoka Marekani kupitia USAID.

Kenya ilipata zaidi ya dola milioni 702 , Rwanda zaidi ya dola milioni 126, Tanzania zaidi ya dola milioni 454, Somalia zaidi ya dola bilioni 1.

Sudan Kusini ilipata zaidi ya dola milioni 800 na Sudan zaidi ya dola milioni 560.

USAID imesimamisha mikataba, ruzuku na makubaliano ya ushirika yanayosababisha kutokuwa na uhakika wa siku 60 hadi 90 kwa misaada tofauti barani.

" Katika Mwaka wa Fedha wa 2024, Marekani ilitoa karibu dola bilioni 6.6 kwa misaada kote Afrika," USAID imesema katika tovuti yake.

Miongoni mwa maeneo ambayo Marekani ina jukumu muhimu ni Sudan iliyokumbwa na njaa, ambapo watu wasiopungua milioni 24.6 wanahitaji msaada wa haraka wa chakula, kulingana na ripoti ya Disemba 2024 ya shirika la kuhakikisha upatikanaji wa chakula duniani.

Marekani ilitoa asilimia 45 ya misaada kwa Sudan mwaka 2024, hii ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

"Upungufu wowote wa ufadhili bila shaka utaathiri watu walio hatarini zaidi wanaotegemea misaada nchini Sudan," alisema msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Misaada kwa watu (OCHA).

Changamoto kwa Uganda

Kwa Uganda takriban dola bilioni 1.5 zimezuiliwa na USAID.

Msaada hii huenda katika kusaidia sekta za afya hasa huduma zinazohusiana na maradhi ya ukimwi, sekta ya kilimo, elimu na msaada kwa watu.

Mwaka wa 2023 , USAID ilitumia zaidi ya dola milioni 500 kwa miradi nchini humo.

Wizara ya Afya nchini Uganda imesema hata kama Marekani imesitisha bado kuna mashirika mengine ya misaada kama Global Fund na GAVI.

" Hii pia inatupa fursa ya kukaa mezani na kuona ni shughuli gani muhimu ambazo hatuwezi kuahirisha na serikali lazima iingie na kuziba pengo hilo, " Diana Atwine, Katibu Mkuu katika wizara ya afya Uganda amesema.

TRT Afrika