Wanajeshi waliopindua serikali ya Niger wamekanusha kuwafukuza mabalozi wengine  / Picha: AFP  / Photo: AFP Archive

Wizara ya Mambo ya Nje ya Niger imeiambia serikali ya Marekani kwamba barua zinazosambaa mtandaoni zikitaka baadhi ya wanadiplomasia wa Marekani kuondoka hazikutolewa na wizara hiyo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema.

"Hakuna ombi kama hilo ambalo limetolewa kwa serikali ya Marekani," msemaji huyo alisema baada ya AFP kuripoti kuwa Niger ilimpa balozi wa Marekani saa 48 kuondoka katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Maelezo kama hayo pia yamesemekana kuwa ghushi baada ya wizara ya nje ya Niger kukanusha habari za kumfukuza balozi wa Ujerumani nchini humo.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Reuters,taarifa zilizochapishwa na shirika la AFP kuwa watawala wa kijeshi wa Niger wamempa balozi wa Ujerumani saa 48 kuondoka, hazikuwa kweli na kuwa Shirika La AFP limeondoa taarifa hiyo mtandaoni mwake na kuweka maelezo kuwa "tumeondoa taarifa hiyo kutokana na kuwa sio sahihi na hayana uthibitisho".

Hii ilitokana na taarifa za awali Ijumaa kuwa Balozi wa Ufaransa nchini Niger, Sylvain Itte, alipewa saa 48 kuondoka nchini humo

Marekani imekuwa ikishinikiza kutatuliwa kidiplomasia mzozo huo uliozuka Julai 26 wakati maafisa wa jeshi la Niger walipochukua mamlaka, kumwondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum na kumweka chini ya kifungo cha nyumbani.

Balozi mpya wa Marekani nchini Niger Kathleen Fitzgibbons aliwasili tu katika mji mkuu, Niamey, mapema mwezi huu.

Reuters
TRT Afrika