Kiongozi wa kijeshi wa Mali Kanali Assimi Goita ametangaza katiba mpya ya nchi hiyo kufuatia kura ya maoni mwezi uliopita.
Kutangazwa kwa katiba mpya katika gazeti rasmi la serikali siku ya Jumamosi na Goita kulikuja siku moja baada ya Mahakama ya Kikatiba ya Mali kuidhinisha matokeo ya mwisho ya kura ya maoni kuhusu rasimu ya katiba.
Junta ya kijeshi hapo awali ilisema kupitisha katiba mpya kutafungua njia ya uchaguzi na kurejea kwa utawala wa kiraia.
Uchaguzi ulitarajiwa kufanywa mnamo Februari 2022, lakini ukaahirishwa hadi Februari 2024.
Tangu kuchukua mamlaka katika mapinduzi ya Agosti 2020, jeshi la Mali limeshikilia kuwa katiba itakuwa muhimu katika kujenga upya nchi.
Katika kuthibitisha matokeo ya mwisho ya kura hiyo ya maoni, mahakama ilikataa maoni ya upinzani ya kutaka matokeo yafutiliwe mbali kwa madai ya "ukiukaji sheria na ukosefu wa upigaji kura katika maeneo kadhaa ya nchi."
Mali ilishuhudia mapinduzi mawili yaliyofuatana katika miaka ya hivi karibuni, moja mnamo Agosti 2020 na nyingine Mei 2021.