Mashirika ya kibinadamu yametoa wito wa msaada wa dharura kufuatia Mafuriko ya hivi majuzi Kaskazini Mashariki mwa Nigeria yaliyosababisha watu wasiopungua 50,000 kuyahama makazi yao tangu mwisho wa juma.
Katika eneo la Sahel na Ziwa Chad, mafuriko makubwa yamezidisha majanga ya kibinadamu yanayoendela katika nchi kama vile Cameroon, Mali na Niger.
"Hali katika ukanda wa Sahel na Ziwa Chad inazidi kuwa mbaya, kwani athari kubwa za migogoro, uhamiaji makazi na mabadiliko ya hali ya hewa yanaathiri sana watu waliyoko hatarini, "alisema Hassane Hamadou, mkurugenzi wa kanda ya Afrika ya Kati na Magharibi wa shirika la Norwegian Refugee Council, NRC.
"Kipaumbele chetu ni kuhakikisha watu walioathirika katika eneo lote wanapokea msaada muhimu kama vile makazi, chakula, na vifaa vya usafi. Suluhu za muda mrefu ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu iliyopo lazima ziratibiwe na serikali za mitaa ili kujenga uwezo wa kukabiliana na majanga yajayo,” ameongezea.
Katika nchi kama vile Cameroon na Niger, jamii ziliyoko kandokando ya Bonde la ziwa Chad, ambazo tayari zinakabiliwa na migogoro na uhamaji kutokana na ukosefu wa usalama, zinakabiliana na tishio la majanga yanayohusiana na hali ya hewa.
Mashirika ya kibinadamu yanasema mafuriko makubwa sasa yanaongezeka mara kwa mara, na athari mbaya za kibinadamu zinatokea karibu kila mwaka. Mashamba katika eneo lote muhimu kwa uchumi wa ndani na usalama wa chakula, yameharibiwa na mafuriko, na kutishia maisha.
Mafuriko hayo pia yameathiri upatikanaji wa elimu kwani shule zimeharibiwa, kulazimishwa kufungwa, au zinatumiwa kama makazi ya muda ya kuhifadhi jamii zilizoathiriwa.
"Tulipoteza sehemu kubwa ya riziki yetu katika maji, na kasi ya mtiririko haikuturuhusu kuchukua mali yoyote muhimu," alisema Modu, mwanamume aliyeathiriwa na mafuriko huko Maiduguri, Nigeria.
"Kwa sasa ninasaidia waathiriwa wengine wa mafuriko, haswa wale ambao hawana makazi mbadala, kuelekea eneo salama. Sote kwa sasa tunaangalia jinsi nyumba zetu zinavyofurika na hakuna tunachoweza kufanya kuhusu hilo.”
Nchini Mali, ambapo msimu wa upungufu wa kilimo umesukuma jamii nyingi kwenye ukingo wa njaa, familia ambazo zinategemea kilimo na ufugaji ili kujikimu zimepoteza kila kitu.
NRC inasema msaada wa haraka unahitajika ili kuzuia hali kuzoroteka zaidi.