Na Coletta Wanjohi
TRT Afrika, Istanbul Uturuki
Mwezi Mei mwaka huu, familia ya Mkenya Joshua Cheruiyot aliyefariki wakati akipanda Mlima Everest iliamua kuuacha kutouzika mwili wa ndugu yao na kuuacha mlimani.
Mlima Everest unakadiriwa kuwa kilele cha juu kabisa duniani ukiwa unafika mita 8849 ambayo ni sawa na futi 29,032.
Unapatikana kati ya Nepal na Tibet katika safu ya milima ya Himalaya.
Marehemu Cheruiyot alifariki akiwa amebakisha mita 48 tu kufika katika kilele cha mlima, na angevunja rekodi ya kupanda mlima huo bila usaidizi wa hewa ya ziada.
Lakini, kwa nini wengi wameshindwa kuchukua miili ya ndugu zao waliofariki katika mlima huo?
Takwimu zinaonyesha, zaidi ya watu 300 wamekufa wakijaribu kuukwea mlima Everest, na zaidi ya miili 200 imebaki huko, na haijaweza kuondolewa.
Katika mlima huu, kuna eneo linaitwa “Death Zone,” yani “Eneo la Kifo". Hili ni eneo lenye urefu wa mita 8,000.
Wapandaji wengi wanapata changamoto kubwa wanapofika katika eneo hili kutokana na baridi kali na viwango vya chini vya oksijeni.
Wanapofika katika eneo la kifo, wanatakiwa kuwa macho katika kufuatilia ustawi wao wa kimwili na hali ya akili ili kupunguza hatari ya kupoteza maisha.
Hivyo, ikitokea mtu amekufa katika eneo hili, inakuwa ni vigumu zaidi kubeba miili iliyoganda, ambayo inaweza kuwa na uzito wa zaidi ya kilo 136.
Watu mara nyingi huuliza kwa nini helikopta hazitumiwi kuhamisha miili katika eneo hilo la mlima.
Hii ni kwa sababu ya muinuko wa juu kabisa ambao helikopta zinaweza kutua kwa uhakika ni kambi ya pili katika mlima huo ambayo ipo kwenye mita 6,400.
Kwa upande mwengine, uokoaji kwa kutumia helikopta na jitihada ya utafutaji wa miili ni changamoto kutokana na urefu na hali ya hewa inayobadilika mara kwa mara.
Pia inaweza kugharimu hadi $70,000 ambayo watu wengi hawawezi kudumu. Na pia inaweza kuwa hatari kwa hata wale wanaokwenda kuondoa miili hiyo, kwa sababu kumekuwa na taarifa mara kadha za waokoaji mwenyewe kupoteza maisha.
Hivyo basi, miili hii inayobaki mlimani, imegeuka sasa kuwa alama kwa wapandaji mlima.
Hii ni kwa sababu, miili haiozi kutokana na uwepo wa barafu. Mwili mmoja maarufu ulikuwa wa mpandaji aliyeitwa "Green boots." Aliaminika alifariki mlimani 1996.
Amekuwa akiitwa hivi kwa sababu alikuwa amevaa viatu vya kijani.
Kwa hivyo, wapandaji walikuwa wanamtumia kama kiekelezo, mfano utasikia watu wakisema, "Ukipita hapo kwenye viatu vya kijani pumzika."
Kuukwea mlima Everest ni jambo la kifahari kwa wale wachache wanaoweza kwani inaweza kugharimu kati ya dola 35,000 na dola 100,000.
Idadi kubwa ya wapandaji wa Everest hutumia oksijeni ya chupa kupunguza athari ya hewa pindi wanapopanda.
Hata hivyo, oksijeni ya chupa ina hatari zake. Kwa kuanzia, ni ghali na ni nzito kubeba.
Pia oksijeni hiyo kwa mfano ikiisha siku ya kufika kileleni, basi mwili wako hauwezi kustahimili upungufu wa ghafla wa oksijeni.
Kwa hivyo, wanaokwea Mlima Everest, tayari wanakuwa wamejianda kisaikolojia kwamba iwapo watakufa mlimani, basi watakuwa wakazi wa kudumu wa Mlima Everest.