Na Brian Okoth
Waafrika wengi walijua meli ya 'Titanic' kutoka kwa filamu ya " The Titanic" ambayo ilkuwa maarufu kuanzia mwaka wa1997.
Ilikuwa hadithi ya kusisimua ya wapenzi wawili ambao walikutana kwa meli hiyo mpya na ya kifahari duniani, msisimuko wa filamu ulikuwa meli ilipozama mwanamke alibaki hai huku mpenziwe akiaga wakiwa wameshikana mkono.
Kwa Uhakika meli ya Titanic - iliyokuwa ikielekea New York City (Marekani) kutoka Southampton (Uingereza) - ilikuwa na watu 2,228 ilipozama mnamo Aprili 15, 1912.
Meli hiyo, iliyokuwa katika safari yake ya kwanza, iligonga jiwe la barafu na kuzama, ikishuka polepole hadi kwenye sakafu ya bahari, takriban kilomita 600 kusini mashariki mwa pwani ya Newfoundland nchini Kanada. Watu 1,508 walikufa katika ajali hiyo.
Kando na uzito wa zaidi ya watu 2,000 na mizigo yao, Titanic ilikuwa imesheheni kilo 39,000 za nyama, kilo 2,400 za mayai, kilo 1,600 za vitunguu, kilo 5,350 za tufaha na kilo 800 za ice cream, kulingana na National Geographic.
Ilichukua miaka 73 tangu ajali kufanyika kwa mabaki yake kuonekana baada ya majaribio kadhaa.
Sheria ya Marekani
Muda mfupi baada ya ugunduzi wa Titanic, Bunge la Marekani lilipitisha Sheria ya ukumbusho wa majini ya Titanic ya RMS ya 1986. Sheria hiyo inakataza kuondolewa kwa mabaki hayo kutoka mahali ilipo.
Hata hivyo, inaruhusu watu kufanya "shughuli ndogo za uchunguzi kwa madhumuni ya kuongeza maarifa ya umma juu ya umuhimu wa Titanic kisayansi, kitamaduni na kihistoria."
Marekani na Uingereza ni miongoni mwa nchi ambazo zimetia saini mkataba wa kimataifa wa "kuilinda Titanic dhidi ya uokoaji wa kibiashara", kumaanisha hakuna mtu, taifa au shirika linaloweza kuiondoa kwenye sakafu ya bahari ili kuionyesha kwa manufaa ya kibiashara.
Mwaka 2012, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilipitisha azimio la kuilinda Titanic chini ya mkataba wake.
"Mabaki ya meli ya abiria ya Titanic sasa yatalindwa na mkataba wa UNESCO ambao unalenga kulinda ajali, maeneo, mapango yaliyopambwa na masalia mengine ya kitamaduni chini ya maji," Umoja wa mataifa ilisema Aprili 2012.
Pia kuna changamoto ya gharama ya kutoa mabaki hayo majini.
Makadirio yaliyoandikwa yanaonyesha kuwa kutoa mabaki ya Titanic baharini kungegharimu zaidi ya dola milioni 35.5. Watu wachache wanaweza kutoa kiasi kama hicho cha pesa kwenye zoezi ambalo lina vizuizi vingi, haswa kisheria.