Maelfu ya Wapalestina walishangazwa kuona nyumba zao zilivyoharibiwa huku zikizungukwa na maiti na damu. / Picha:Reuters  

Kusitishwa kwa mapigano kwa muda Gaza, kumeonyesha ukubwa wa janga la kibinadamu na uharibifu mkubwa uliofanywa na jeshi la Israeli katika maeneo tofauti, hasa katika mji wa Gaza na eneo la kaskazini.

Dakika za mwanzo za kusitishwa kwa mapigano, maelfu ya Wapalestina waliokuwa wamehama makazi yao walikwenda kuangalia nyumba zao na majirani, hasa katika eneo la mpakani ambapo jeshi la Israeli lilipelekwa.

Wapalestina wamebaini uharibifu mkubwa uliofanywa na vikosi vya Israeli katika maeneo yao ya makazi.

Miili iliyoharibika

Mashuhuda wameiambia Anadolu kwamba, pindi walipokuwa wanarudi majumbani mwao magharibi mwa mji wa Gaza na katika mji wa Beit Hanoun na Beit Lahia, wameona mamia ya miili ya Wapalestina waliouliwa na jeshi la Israeli.

Wamesema kwamba, miili ilikuwa imeoza, ikiashiria kwamba wameuawa wiki kadhaa zilizopita, aidha kutokana na mashambulizi ya anga au pindi walipokuwa wanaondoka Gaza kuelekea maeneo ya kusini.

Uharibifu mkubwa

Mbali na uharibifu mkubwa wa miundombinu ikiwemo barabara, majengo ya serikali na taasisi binafsi, miundombinu ya maji, umeme na mitambo ya mawasiliano pia imeharibiwa.

Miongoni mwa maeneo ambayo kumeshuhudiwa uharibifu mkubwa ni miji ya Beit Hanoun, Beit Lahia na Jabalia, maeneo jirani ya Al Rimal, Tal Al Hawa, Sheikh Ijlin, na maeneo ya majengo ya Hospitali ya Al Shifa katika mji wa Gaza.

Vikosi vya uokoaji vimeanza kazi yao ya kukusanya maiti kutoka katika majengo yaliyoharibiwa, hayo ni kwa mujibu wa mashuhuda.

Washuhudia janga

Suhail Abdel Nabi, Mpalestina kutoka Bir al Naja katika mji wa Jabalia, amesema kwamba yeye alishangazwa alipogundua kwamba nyumba yake imebomolewa. Aliiacha ikiwa katika hali nzuri wiki mbili zilizopita pindi alipokimbia eneo hilo kwenda eneo la jirani la Al Tuffah, mashariki mwa mji wa Gaza.

“Niliondoka kwa mguu asubuhi hiyo kutoka katika moja ya shule nilipokuwa na familia yangu jirani na Al Tuffah, na saa mbili baadae nilifika na kuona nyumba yangu imeharibiwa kabisa,” ameiambia Anadolu.

"Tumeona miili ya waliokufa mashahidi katika eneo letu. Hawa ni ndugu zetu ambao walijaribu kukimbia siku chache zilizopita, lakini walilengwa na jeshi la Israeli na mizinga yao," ameendelea kusema.

Vikosi vya Israeli bado vipi Gaza

Magari ya jeshi la Israeli yameweka kambi katika eneo la barabara ya Al Rashid kuelekea Kaskazini mwa Mkoa wa Gaza katika mji wa Gaza, hii ni mbali na uwepo wao katika eneo la kusini la Al Zaytoun na Sheikh Ijlin.

Jeshi la Israeli liliendelea na mashambulizi ya ardhini katika maeneo ya mji wa Beit Hanoun, Beit Lahia na Jabalia, kwa mujibu wa vyanzo vya ndani.

TRT Afrika