Krismas

Evarist Mapesa

TRT Afrika, Mwanza, Tanzania

Waumini wa dini ya Kikristo nchini Tanzania wameungana na Wakristo ulimwenguni kote kusheherekea sikukuu ya Krismas ambayo kwao ni ishara ya kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Siku hii imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka ifikapo December 25, ambapo hutanguliwa na mkesha wa Krismas huku shughuli mbalimbali za kidini zikifanyika ikiwemo ubatizo kwa baadhi ya madhehebu.

waumin

Kila ifikapo December 25, Wakristo huiumia siku hii kama sherehe na siku maalumu ambapo watu hupika chakula cha kila aina, huku wakinywa na kuburudika.

Kwa kawaida mitaa mbalimbali hupambwa, miziki ya kila aina ikipigwa, watu huburudika, watoto hutembea katika maeneo tofauti huku wazazi pia wakifurahia siku hii kwa kupumzika na familia zao.

Wakristo wanasherehekeaje siku hii?

Wakristo wengi wanapotoka kusali ibada ya Krismas hujumuika na familia zao kwenye chakula cha mchana, na usiku huku wakitumia vinywaji mbalimbali kusukuma burudani na furaha yao juu ya siku hii.

Diana Trazius ni mkazi wa Mwanza magharibi mwa Tanzania, anaiona siku hii kuwa ya kipekee katika maisha yake licha ya kuwa ameshuhudia sikukuu za Krismas nyingi tangu alipozaliwa.

“Namshukuru Mungu kwa kusheherekea sikukuu ya mwaka huu, ni Krismas ambayo inaonesha kwamba ina uhai ndani yake kwa sababu imepita miaka mingi, lakini mambo mengi yametokea, tunaona huko Hanang wamepata mafuriko, lakini Mungu ametulinda sisi watu wa Mwanza.”

“Kwa hiyo kipekee namshukuru Mungu kufikia siku hii ya leo, lakini pia nitaendaje kuisherehekea sikukuu yangu, mimi binafsi nitakuwa nyumbani kuisherehekea sikukuu hii,” amesema Trazius.

Krismas

Aman Victor anasema Krismas kwa upande wake ameipokea vizuri, kutokana na utamaduni wa sherehe hiyo ya kidini kufanyika kila mwaka, “Nimeipokea vizuri sana, kwa sababu ni muendelezo wa kile ambacho tumekuwa tukikifanya miaka yote, kwa upande wangu ninaisherehekea na familia ambayo nipo nayo nyumbani, na wazazi wangu, wadogo zangu, kwa hiyo nitaisherehekea kwa namna hiyo mimi na familia yangu.”

Changamoto katika kipindi hiki

Maandalizi ya sherehe za mwisho wa mwaka huanza mapema kwa watu kuanza kutunza kiasi fulani cha fedha ili kiwasaidie kununua baadhi ya mahitaji kama nguo, vyakula na vinywaji katika sikukuu za Krismas na mwaka mpya.

Victor, ameiambia TRT Afrika kwamba katika kipindi cha mwaka 2023, moja ya changamoto kubwa aliyoipitia ilikuwa ni mdororo wa kiuchumi na kusababisha kushindwa wakati mwingine kupata chakula cha siku.

"Tunasherehekea sikukuu hii mwaka huu wa 2023, lakini changamoto kubwa niliyokutana nayo ni ya kiuchumi, kuna muda ilifikia nikayumba kidogo lakini Mungu ni mwema naona mambo yamerudi kama kawaida," anasema Victor.

Viongozi watoa ujumbe gani?

'Nyoyo yetu ziko Bethlehem': Papa Francis

Wakati akiongoza misa ya Mkesha wa Krismas kwenye kanisa kuu la St. Peter's Basilica, Vatican, Papa Francis ameitisha amani huku mapigano ya Israeli dhidi ya Gaza yakiendelea kupamba moto huko Palestina.

"Usiku wa leo, nyoyo zetu ziko Bethlehem, ambapo amani inakataliwa na fikra za vita,” aliwaambia waumini takriban 6,500."

Wakati huo huo, viongozi mbalimbali wa nchi za Kiafrika walitumia mtandao wa kijamii wa X, zamani Twitter kutoa salam zao la sikukuu.

Kikubwa, marais hao waliwataka wananchi wao kuzingatia amani, utulivu na umoja katika sherehe hizo za kuelekea mwaka 2024. huku baadhi wakikumbuka matukio makubwa yaliyotokea mwaka 2023.

Bola Tinubu wa Nigeria

"Wacha mwanga wa Krismas uongoze njia yetu tukielekea kuumaliza mwaka huu na kuukaribisha mwaka mpya. Nigeria muda mfupi itaibuka katika maendeleo na amani."

Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini

"Tunawashukuru wote kutoka pande zote ambao wamepambana kuifanya nchi yetu yenye uhuru, usawa na maedeleo, ambapo hakuna aliyeachwa nyuma. Tunauangalia mwaka ujao kwa matumaini. Tuendelee kupambana kwa kuleta ubinadamu, na upendo ambao unatufanya tuwe hivi tulivyo."

William Ruto wa Kenya

"Tunapokusanyika na familia zetu na jamii zetu, tuwafikie ndugu zetu wenye kuhitaji upendo, maneno mazuri, chakula kizuri na zawadi nyengine."

Samia Suluhu wa Tanzania

"Katika msimu huu wa sikukuu, wengi wenu wanasafiri kuelekea sehemu mbalimbali kukutana na familia zenu na marafiki, nawataka mfuate sheria za barabarani na uangalifu ili wiki hii iwe ya furaha kwetu sote."

Yoweri Museveni wa Uganda

"Tunamshukuru Mungu kwa kutufikisha hapa na kukaribia kukamilisha mwaka. Heri ya Krismasi.!"

TRT Afrika