Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amekashifiwa kwa kuweka siri uamuzi wa serikali yake wa kutuma takriban vijana 221 kufanya kazi katika mashamba nchini Israel.
Kusafirishwa kwa vijana hao na ndege ya Israel Airbus A321-251 usiku wa Jumamosi kumewakasirisha Wamalawi wengi. Hatua hiyo inafuatia msaada wa dola milioni 60 kutoka Israel hadi Malawi wiki mbili zilizopita.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Leba, Kazi Wezi Kayira alisema kusafirisha vibarua katika nchi mbalimbali, ikiwamo Israel, ni njia mojawapo ya kutengeneza ajira kwa vijana na kuingiza fedha za kigeni kwa taifa hilo la kusini mashariki mwa Afrika ambalo lina wakazi milioni 20.
“Mpango huu utanufaisha watu binafsi na taifa. Sehemu ya mishahara itagharamia maisha yao nchini Israel huku iliyobaki itatumwa kwa akaunti za kibinafsi hapa Malawi ili kuongeza fedha za kigeni,” Kayira alisema katika taarifa iliyoshirikiwa na Anadolu.
Vijana 'hawataajiriwa kupigana'
Pia alisisitiza kwamba vijana wa Malawi hawatapigana katika vita vya Israel dhidi ya kundi la Hamas la Palestina, lakini "watafanya kazi katika maeneo yaliyoidhinishwa , ambayo yameainishwa kama mazingira yanayofaa na salama."
Hata hivyo, Gift Trapence, mwenyekiti wa Muungano wa Watetezi wa Haki za Binadamu, kikundi cha haki za kiraia, alihoji usiri unaozunguka mkataba wa mauzo ya kazi na Israel.
“Tunalaani seŕikali kwa kuwa msiri katika mkataba wa mauzo ya nje ya kazi ambayo imeingia na Israel. Vitendo vya serikali kuhusu usafirishaji wa wafanyikazi nchini Israeli vinapaswa kuwa wazi," Trapence aliiambia Anadolu.
Kiongozi wa upinzani katika bunge la Malawi, Kondwani Nankhumwa, ambaye alizungumzia suala hilo kwa mara ya kwanza bungeni siku ya Alhamisi, aliiambia Anadolu kwa njia ya simu kwamba serikali ilichagua kuweka suala hilo kuwa siri kwa sababu inajua huu ni "muamala mbaya."
Hakuna ‘mzazi mwenye akili timamu’ anayeweza kumpeleka mtoto Israeli
“Serikali imeingia katika makubaliano hayo na makampuni ya Israel wakati inafahamu kikamilifu kuwa kuna vita. Hakuna mzazi mwenye akili timamu anayeweza kumtuma mtoto wake kufanya kazi katika nchi ambayo iko vitani,” Nankhumwa alisema.
Wizara ya kilimo ya Israel imerekodiwa kusema kuwa kati ya wafanyakazi 30,000 na 40,000 wameondoka katika mashamba ya nchi hiyo, nusu yao wakiwa ni Wapalestina ambao walizuiwa kuingia Israel kutoka Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu tangu mashambulizi ya Oktoba 7.
Wakati huo huo, serikali ya Israel inatazamia kuajiri baadhi ya wafanyakazi 5,000 kutoka nchi nyingine, ikiwa ni pamoja na Malawi.