Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya imesema kuwa ipo tayari kuunga mkono juhudi za upatikanaji amani nchini Sudan.
Uthibitisho huo unakuja siku moja baada ya Sudan kuituhumu Kenya kwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa wanajeshi wa RSF, jijini Nairobi.
Katika taarifa yake, Sudan imedai kuwa hatua ya Kenya kuandaa mkutano huo ni ya ‘kichokozi’.
Naibu Kamanda wa RSF Abdel-Rahim Hamdan Dagalo aliongoza ujumbe wa Sudan katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta ulioko jijini Nairobi.
Kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, Kenya ina historia ya kuandaa mazungumzo ya amani pamoja na kuwapokea wakimbizi kutoka Sudan.
Hata hivyo, profesa wa masuala ya ushirikiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha USIU Macharia Munene, alionya kuwa Kenya iko katika hatari ya kutengwa kimataifa kutokana na “makosa katika sera za mambo ya nje."
Kulingana na Profesa Munene, sera ya mambo ya nje ya Kenya “imekuwa ikiendeshwa na mtu mmoja” huku Rais wa nchi hiyo akitumia faida ya urafiki wake na kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo, ambaye pia hujulikana kama Hemedti, bila kujali “maslahi ya Kenya kama taifa.”
Licha ya kutokuwepo kwenye tukio hilo la Jumanne, Hemedti anajulikana kuwa mtu wa karibu wa Rais William Ruto huku ndugu yake akiwa amekutana na Rais huyo mara kadhaa.
Mgogoro unaoendelea nchini Sudan umesababisha vifo vya watu zaidi 24,000 na kuwafanya wengine milioni 14 kukosa makazi, kulingana na Umoja wa Mataifa.