Kenya imetangaza kuondoleana hitaji la viza ya usafiri na Angola kama njia ya kuimarisha uhusiano wa kibaishara na Utalii kati ya nchi hizo mbili.
Katika ziara ya kwanza kabisa ya ngazi ya juu kutoka Angola Rais João Lourenço alisaini mikataba kumi na moja ya makubaliano na mwenyeji wake William Ruto, ikiwemo kilimo, biashara, jiolojia, uwekezaji, misitu, huduma ya umma miongoni mwa zinginezo.
Makubaliano hayo ya kuondolewa viza kati yao yanasubiri kuthibitishwa kutoka upande wa Angola pindi tu Rais Lourenço atakaporejea nchini mwake na kuweka itifaki sawa.
"Ndugu na dada zetu nchini Angola walio na hati za kusafiria sasa hawatahitaji visa kuja Kenya. Nina furaha sana kwamba rais wa Angola pia atazingatia vivyo hivyo atakaporejea nyumbani,” alisema Rais Ruto.
Angola inaunga orodha ya orodha inayoonekana kuendelea kukua ya mataifa ya Afrika yaliyoondolewa hitaji la viza kusafiri nchini Kenya.
Miongoni mwa nchi zilizoondolewa Visa kusafiri Kenya hivi karibuni ni Afrika Kusini, Eritrea na Comorros.
Tangu kuingia madarakani Rais Ruto amekuwa akiuza azma yake ya kuifanya Afrika kuwa huru kwa usafiri miongoni mwa Waafrika, akisema kuwa itawezesha wananchi wa bara hilo kusafiri, kufanya biashara, kubadilishana utamaduni na mitazamo.
''Tumejadiliana pia namna ya kuharakisha na kutamatisha mashauriano juu ya ufunguzi wa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Kenya na Angola, kama njia ya kuimarisha uhusiano huu wa kibiashara, ambao umekua kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni'' aliongeza Rais Ruto.
Rais Ruto alisema kuwa biashara kati ya nchi hizo imekuwa kutoka dola milioni 60 hadi dola milioni 350 katika muda wa miaka minne kufikia mwaka 2022.
''Tunataka kuona idadi hiyo ikifikia mabilioni ya dola, na tutafanya kila juhudi nchini ya makubaliano baina ya nchi hizi.'' Alisema Rais Ruto.
Kwa upande wake Rais wa Angola alipongeza hatua ya Kenya ya kuonyesha undugu usio na kifani.
'Na sisi upande wetu tutakaporudi nyumbani tunakuhakikishia kuwa tutajadili kwa kina pendekezo lako la kuondoa viza na tutalifanikisha.' alisema rais Lourenço.
Rais Lourenço alisema Kenya na Angola zinashirikiana katika kuleta amani katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kuwa wamekubaliana kuimarisha juhudi hizo.
'Tumekuwa tukifanya kazi pamoja kuhusu suala nyeti la uslama wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo. Japo ni suala lenye misukosuko, na changamoto nyingi, bado linawezekana.'' alisema Rais Lourenço.
Rais João Lourenço ameandamana na mke wake mheshimiwa Ana Dias Lourenço, viongozi wa serikali yake wakiwemo mawaziri na ujumbe wa wafanya biashara kwa ziara ya siku tatu nchini Kenya.