Vita vimepamba moto kati ya vikosi vya jeshi la Sudan na Vikosi vya RSF, tangu Aprili 2023/ Picha: Wengine

Kamati ya wanaharakati nchini Sudan ilisema watu 31 waliuwawa katika shambulio la anga la kijeshi kwenye msikiti mmoja kwenye mji wa Wad Madani, ulio katikati ya nchi ya Sudan.

Shambulio hilo lilitokea "baada ya sala ya jioni" siku ya Jumapili katika mji mkuu wa jimbo la Al-Jazira kusini mwa Khartoum, Kamati ya Upinzani ya Wad Madani, moja ya vikundi vinavyojitolea kuratibu misaada nchini Sudan, kilisema katika taarifa yake iliyonukuliwa na Shrika la Habari la AFP, mapema Jumanne.

Walishutumu jeshi kwa kutumia "mabomu", na kuongeza kuwa zaidi ya nusu ya waliofariki bado hawajatambuliwa huku waokoaji wakipitia mabaki ya "miili kadhaa iliyoungua na kukatwakatwa".

Vita nchini Sudan vinazidi kupamba moto, huku vikihusisha Jeshi la Sudan dhidi ya RSF tangu kuibuka kwa mgogoro wa kisiasa Aprili 2023.

Vikosi hivyo viwili viko katika mapigano makali ya kuwania eneo la Al-Jazira, ambalo liko chini ya udhibiti wa wanajeshi tangu mwishoni mwa mwaka jana.

Pande zote mbili zimeshutumiwa kwa uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na kuwalenga raia, kupiga makombora kiholela katika maeneo ya makazi, kuzuia usambazaji wa misaada pamoja na kuipora.

TRT Afrika