Zaidi ya watu milioni wameathiriwa na mafuriko Sudan Kusini, kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA).
Mafuriko hayo yamewaacha watu wapatao 271,000 bila ya makazi, huku wengine wakilazimika kutafuta hifadhi kwenye maeneo ya mbali, limesema shirika hilo.
OCHA imesema kuwa mvua kubwa zilizoshuhudiwa eneo hilo limezorotesha usambazaji wa misaada ya kibinadamu.
Sudan Kusini, ambalo ni taifa changa kabisa duniani, linakabiliwa na mafuriko mabaya zaidi kupata kushuhudiwa kwa miongo kadhaa, yakiwa yamesababisha uharibifu wa miondombinu na maisha ya watu.
Siku ya Jumatatu, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilisema kuwa mafuriko hayo yaliathiri hali ya kibinadamu nchini Sudan Kusini, ambapo kwa sasa kuna wakimbizi wapatao 800,000 waliokimbia machafuko nchi ya jirani.