Na Emmanuel Onyango and Najib Bencherif
Operesheni za kikundi cha Wagner barani Afrika zimekuwa zikiangaziwa sana kufuatia uasi yake ya muda mfupi nchini Urusi ambayo yalisababisha kiongozi wake, Yevgeny Prigozhin, kuambiwa ahamie Belarus.
Kundi hilo la mamluki limekuwa na nyayo katika nchi sita za Kiafrika - Msumbiji, Madagascar, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Sudan, Mali na Libya.
Katika nchi hizi wapiganaji wake elfu kadhaa wamefanya kazi chini ya kandarasi za usalama zinazohusisha mapigano au mafunzo ya maofisa wa usalama wa serikali.
Kwa upande wa nguvu za kijeshi, kundi la Wagner linaaminika kuwa na wapiganaji wapatao 5000 wanaofanya kazi barani Afrika.
Shughuli zake zilianza 2017 na zimekuwa zikipanuka tangu wakati huo.
Ikiahidi kutoa usalama, kikundi cha Wagner kilipata leseni katika ya tasnia za uchimbaji madini ya almasi na dhahabu pamoja na kunufaika na mafuta.
Kupitia mtindo huo wa biashara, kikundi cha Wagner kimeonekana kikilinda mali za kiuchumi nchini Libya ikiwa ni pamoja na visima vya mafuta katika ngome za jenerali muasi Khalifa Haftar.
Nchini Msumbiji wamepambana na waasi katika jimbo lenye utajiri wa mafuta la Cabo Delgado ambako pia walipata majeruhi.
Haki za binadamu
“Hawapo kwa sababu wanawajibika kwa jamii, wapo kwa sababu wanataka kupata pesa. Wanafanya chochote kinachohitajika ili kupata pesa na hiyo ndivyo historia ya kundi la Wagner barani Afrika," Thembisa Fakude, Mkurugenzi wa Africa Asia Dialogues Institution, aliiambia TRT Afrika.
Operesheni nyingi za Wagner katika bara hilo zilitegemea udhamini wa Urusi na ikawa chombo muhimu katika ushawishi wa Kremlin barani Afrika.
Hii ilikuwa haswa katika nchi zisizo na utulivu ambapo mipango inayoongozwa na Ufaransa ilishindwa kurejesha utulivu.
Nchini Mali, kuwasili kwa kundi la Wagner mnamo 2021 baada ya jeshi kunyakua mamlaka kulikaribishwa na umati wa watu wenye shangwe ambao walipeperusha bendera za Urusi na kubeba mabango ya kukemea ukoloni wa zamani wa Ufaransa.
Iliripotiwa kikundi hicho kilikuwa kinalipwa takriban dola milioni 11 kwa mwezi kwa huduma zake huko, kulingana na mashirika ya habari.
Wapiganaji wake hivi karibuni walishtakiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu nchini ikiwa ni pamoja na katika mikoa ya Mopti, Segou, Tombouctou, na Koulikoro, kulingana na data ya Armed Conflict Location and Event Data Project (ACLED).
Ni uamuzi wa Afrika
Shutuma kama hizo za dhuluma dhidi ya raia zilitolewa kwenye oparesheni za Wagner katika Jamhuri ya Afrika ya kati, ambapo ilisaidia serikali ya rais Faustin-Archange Touadéra kujikinga na muungano wenye nguvu wa waasi ambao ulitaka kuchukua madaraka.
Lakini wachambuzi wengine wanaamini baadhi ya simulizi dhidi ya kundi la Wagner zinaegemea upande mmoja.
"Masimulizi yanayopendekezwa ni kwamba kila wanachogusa ni janga kamili na sidhani kama kuna ushahidi wa hilo," Alex Vines, Mkurugenzi wa Mpango wa Afrika katika shirika la Chatham House, aliiambia TRT Afrika.
"Masimulizi ya Magharibi ni kwamba kila kitu ambacho Wagner wamefanya ni cha kutisha - ukiukwaji mwingi wa haki za binadamu. Operesheni zao zilishindwa Msumbiji, hawajafanikiwa nchini Mali. Lakini wamefanikiwa kwa namna fulani katika kutoa aina fulani ya usalama ndani ya mzozo wa ndani nchini Libya kwa mfano,” Vines amesema.
Wagner hajaonyesha nia yoyote ya kusitisha uhusiano wake na nchi za Afrika lakini maswali yanasalia kutokana na uasi wa wiki iliyopita.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov alikuwa amehakikisha kwamba mikataba ya usalama ya kundi hilo itasalia. Ingawa baadaye walisema kwamba viongozi wa nchi za Afrika wanapaswa kuamua kama wanataka kuendelea kufanya kazi na Wagner.
Marekani imesema itatangaza hatua zaidi za kuwawajibisha kundi hilo kwa shughuli zake barani Afrika.
Athari tofauti
Wengine wanawaza kuwa mvutano kati ya uongozi wa kundi la Wagner na serikali ya Urusi chini ya rais Vladmir Putin unaweza kuja na athari tofauti kwa operesheni za kundi hilo barani Afrika.
‘’Ni habari njema kwa Afrika kwa sababu Wagner Group haijaleta mabadiliko ya kuvutia katika ushiriki wake barani Afrika. Haitakuwa vizuri kwa nchi kama vile Mali ambayo inaegemea kundi la Wagner katika kupambana na wanamgambo, inawaacha katika mazingira magumu,” alisema Fakude.
"Maeneo mengine kama Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR tunapaswa kusubiri na kuona, ikiwa ni pamoja na nchi kama Msumbiji, DRC na maeneo mengine ya Afrika ambako wagner wako."
Lakini katikati ya sintofahamu kuna maswali kuhusu namna ambavyo kuondoka kwa Wagner barani Afrika kutaathiri hasa juu ya utulivu katika Sahel, ambapo waasi wanaweza kutafuta fursa ya kurejea katika maeneo walupolazimika kuondoka , na hata kuingia katika maeneo mengine mapya.
Serikali katika mikoa hiyo bado haijatoa maoni yoyote ingawa uasi katika eneo la Sahel hapo awali, umeenea hadi pwani ya Afrika Magharibi.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Mali, unatazamiwa kumaliza majukumu yake na kuanza kuondoka nchini Mali. Hii inafuatia mvutano wa miaka mingi kati ya Umoja wa Mataifa na viongozi wa kijeshi wa Mali.
Kujiondoa kwa kundi la Wagner nchini humo kutamaanisha vikosi vya Mali visivyo na vifaa vya kutosha kupambana na waasi peke yao.
Kwa njia mbadala, baadhi ya wanajeshi wa Kiafrika wanaweza kuingia kuchukua majukumu yaliyotekelezwa na kundi hilo - sawa na kile ambacho majeshi ya Rwanda yanafanya hivi sasa kaskazini mwa Msumbiji.
"Wanajeshi wa Kiafrika wanaweza kushindana na mahitaji wa kifedha ya Wagner pia na nadhani hilo ni jambo zuri. Ni bora kuwa na jeshi la Kiafrika lenye nidhamu linaloshughulikia hili kuliko wageni. Habari kuhusu uwepo wa Rwanda nchini Msumbiji ni nzuri,” anasema Vines.