Mkutano wa marais wa jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS, umeamua kuwa wanajeshi watatumwa nchini Niger ambapo mapinduzi yamekuwepo tangu 26 Julai mwaka huu.
Hii wamesema ni kwa ajili " ya kurejesha hali ya kikatiba" Niger.
Lakini Je, uingiliaji wa kijeshi kutaibadili hali ya serikali Niger?
Solomon Dersso Mkurugenzi Mkuu wa Amani Afrika anasema kuwa kutuma wanajeshi Niger hakuwezi toa uhakikisho wa kumuokoa rais Mohamed Bazoum,
Amani Afrika ni shirika ambalo hufanya utafiti wa amani na usalama na kufanya kazi kwa karibu na Umoja wa Afrika.
" Tuna uhakika gani kwamba wanajeshi wakiingia kupigana na wapinduzi wa Niger ambao pia ni wanajeshi , rais Bazoum hatauawa katika harakati hiyo?" Dersso anauliza.
Rais Mohamed Bazoum bado anashikiliwa na wanajeshi waliofanya mapinduzi tangu 26 Julai.
"Jeshi la jumuiya ya ECOWAS ikiingia , tutajenga amani ama tutaharibu zaidi?" Alain Nyamitwe, balozi wa zamani wa Burundi kwa Umoja wa Afrika anauliza.
"Ni muhimu kurejesha hali ya kikatiba kwa sababu Niger ikiporomoka, nchi nyingi jirani zitaporomoka, " Nyamitwe anasema , " tusisahau Libya baada ya kuuawa kwa rais wa nchi hiyo Ghadaafi, vile vikundi vya silaha vinaathiri eneo hilo na magaidi waliingia nchi jirani na kuanza kufanya uharibifu."
Hofu ni kwamba nchi ya Niger imekumbwa na magaidi ambao pia ni tishio kwa nchi zingine zilizo katika eneo la Sahel.
Wataalam wanasema kuwa kutuma majeshi Niger kutaathiri uwezo wa jeshi la Niger kuilinda nchi yake vizuri na hapo kuwapa magaidi nafasi ya kuingia mazima nchini humo .
" Lakini hii haitaathiri tu Niger , bali majirani wake pia, " anaongezea Dkt Dersso , " nchi kama Nigeria na Algeria ambazo zimepakana na Niger pia zitakuwa katika hatari ya kuingiliwa na magaidi."
Nchi zilizo katika eneo la Sahel ni pamoja na Libya, Burkina Faso, Cameroon, Chad, Gambia, Guinea, Mauritania, Mali, Niger, Nigeria na Senegal.
Changamoto ingine ipo kwa majirani wa Niger ambao wameamua wataunga mkono majeshi yaliyopindua serikali.
"Mali na Burkina Faso tayari zimesema zitaunga mkono Niger kukiwa na uingiliaji wa kijeshi, " Dersso anaongezea, " hii inaleta changamoto ya uwepo wa vita vya kikanda.
Mali , Burkina Faso na Guinea ziko chini ya uongozi wa kijeshi baada ya mapinduzi pia kufanyika katika nchi hizo.
"Nadhani kwamba njia ya kupunguza hatari nchi hiyo na nchi zingine za Afrika ni njia ya diplomasia njia ya mazungumzo , njia ya kuambia yale amajeshi ya kuwa ni vizuri warejeshe rais halali rais Bazoum , hili linawezekana," Balozi Nyamitwe anasema.
Wanajeshi walioongoza mapinduzi Niger wametangaza kuwa wameteua baraza la uongozi wa mpito.
Serikali mpya ya Niger ilitangazwa na Jenerali Abdourahamane Tchiani.
Wamemteua Ali Mahaman Lamine Zeine kama Waziri Mkuu na ataongoza serikali hiyo ya mpito, wenye wanachama 21, huku majenerali kutoka baraza jipya la uongozi wa kijeshi wakiongoza wizara ya ulinzi na mambo ya ndani.