Rais wa farika Kusini Cyril Ramaphosa amesema alikubaliana na marais wa Urusi na Ukraine kuanza maandalizi ya mazungumzo na wakuu wa nchi za Afrika / Photo: AFP

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alisema Jumatatu kuwa ujumbe wa amani kutoka Afrika utatafuta suluhu ya mzozo kati ya Urusi na Ukraine

Ujumbe huo unajumuisha viongozi wa nchi za Afrika, kutoka Zambia, Senegal, Congo, Uganda, Misri na Afrika Kusini.

"Nilikubaliana na Rais Putin na Rais Zelenskyy kuanza na maandalizi ya mazungumzo na wakuu wa Nchi za Afrika," aliambia mkutano na vyombo vya habari.

Dkt. David Matsanga mchambuzi wa kisiasa anaiambia TRT Afrika kwamba itakuwa "muujiza" ikiwa Afrika itatatua mzozo huo.

"Ni kupoteza muda na mazoezi ya bure ambayo hayatazaa matunda," anasema Dk Matsanga. "Tatizo la mzozo wa Ukraine linaweza kutatuliwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, ambapo Urusi na Marekani ni wanachama wa kudumu," anaongeza, "haihitaji nchi ya Kiafrika kupoteza rasilimali za watu wa Afrika."

Afrika haijakuwa na sauti moja kuhusu mzozo wa Russia na Ukraine, huku baadhi wakipiga kura kuunga mkono Urusi au Ukraine kwenye Umoja wa Mataifa na wengine wakichagua kujiepusha na kutounga mkono upande wowote.

Umuhimu wa mkataba wa Bahari Nyeusi baada ya Mgogoro wa Urusi na Ukraine

Moja ya athari za moja kwa moja za vita kati ya Urusi na Ukraine kwa Afrika imekuwa kukatika kwa usambazaji wa bidhaa kutoka Ukraine na Urusi, ambazo ni pamoja na mafuta ya alizeti, ngano na mahindi.

Urusi ni muuzaji mkuu wa kimataifa wa mbolea.

Umoja wa Mataifa unasema mpango wa Bahari Nyeusi umeruhusu usafirishaji salama wa zaidi ya tani milioni 30 ya bidhaa tangu Julai 2022

Benki ya Maendeleo ya Afrika, yaani African Development Bank, inasema mzozo huo umesababisha uhaba wa takriban tani milioni 30 za nafaka barani Afrika.

Juhudi zinaendelea kushinikiza kupanuliwa kwa mkataba wa nafaka wa Bahari Nyeusi ili kuruhusu usafirishaji salama wa nafaka wa Bahari Nyeusi nchini Ukraine.

Mkataba huu ulipitishwa Julai 2022 kati ya Moscow na Kiev na ulisimamiwa na Uturuki kwakushirikiana na Umoja wa Mataifa.

"Mpango wa Black Sea Initiative ulikuwa muhimu sana wakati ambapo Afrika imekuwa ikitegemea Urusi na Ukraine kwa nafaka, na pia bidhaa za viwandani za mbolea zinatoka Urusi na Ukraine," Edward Wanyonyi, mtafiti katika tafiti za usalama na maendeleo anaiambia TRT Afrika,

"kwa kweli ilisaidia hakutakuwa na changamoto za usalama wa chakula barani humo."

Umoja wa Mataifa unasema mpango huo umeruhusu usafirishaji salama wa zaidi ya tani milioni 30 ya bidhaa tangu kuanza kwa mara ya kwanza Julai 2022.

Kituo cha Uratibu wa Pamoja ambacho 'huruhusu meli kusafirisha kwa usalama nafaka , vyakula vingine na mbolea, ikiwa ni pamoja na amonia, kutoka Ukraine kupitia ukanda wa kibinadamu wa baharini' kilianzishwa mnamo tarehe 27 Julai 2022 huko Istanbul.

Mikutano imekuwa ikiendelea kati ya Uturuki, Ukraine, Urusi na Umoja wa Mataifa kuhusu haja ya kuongeza muda wa makubaliano hayo hadi tarehe 18 Mei 2023

"Kuendelea kwa Mpango wa Bahari Nyeusi ni muhimu sana," Martin Griffiths, mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura aliambia mkutano wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Ukraine.

Mwisho wa changamoto hizi na zaidi unategemea sana mzozo wa Russia na Ukraine unaokaribia mwisho, lakini kama ujumbe wa amani wa Afrika ndio utakaoleta matokeo haya ni swala la kungoja na kuona.

TRT Afrika