Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema anataka wahamiaji wa Eritrea waliohusika katika mapigano makali mjini Tel Aviv wafurushwe mara moja na ameamuru mpango wa kuwaondoa wahamiaji wote wa Kiafrika nchini humo.
Matamshi hayo yanajiri siku moja baada ya maandamano ya umwagaji damu ya makundi hasimu ya Waeritrea kusini mwa Tel Aviv na kusababisha makumi ya watu kujeruhiwa.
Raia wa Eritrea, wafuasi na wapinzani wa serikali ya Eritrea, walikabiliana katik amaandamano kwa kutumia mbao za ujenzi, vipande vya chuma na mawe, kuvunja madirisha ya maduka na magari ya polisi.
Polisi wa Israel wakiwa na vifaa vya kutuliza ghasia walifyatua gesi ya kutoa machozi, maguruneti ya kushtukiza na risasi huku maafisa waliokuwa wamepanda farasi wakijaribu kuwadhibiti waandamanaji.
Ghasia hizo siku ya Jumamosi zilifufua suala la wahamiaji, ambalo limeigawanya Israel kwa muda mrefu.
Kuibuka tena kwake kunakuja wakati Israeli inakabiliwa na mpango wa marekebisho wa mahakama wa Netanyahu, na wafuasi wanataja suala la wahamiaji kama sababu ya mahakama kuzuiliwa, wakisema imekuwa kizuizi kikubwa katika mpango wa kuwaondoa wahamiaji hao.
'Hatua kali'
"Tunataka hatua kali dhidi ya wafanya ghasia, ikiwa ni pamoja na kufukuzwa mara moja kwa wale walioshiriki," Netanyahu alisema Jumapili wakati wa mkutano maalum wa mawaziri ulioitishwa kushughulikia athari za ghasia.
Aliomba mawaziri waandae na kumfikishia mipango "ya kuondolewa kwa wahamiaji wengine wote haramu ," na akabainisha katika maelezo yake kwamba Mahakama ya Juu ilifutilia mbali baadhi ya hatua zilizokusudiwa kuwashurutisha wahamiaji hao kuondoka.
Takriban wahamiaji 25,000 wa Kiafrika wanaishi Israel, hasa kutoka Sudan na Eritrea, ambao wanasema walikimbia migogoro au ukandamizaji.
Israel inawatambua wachache sana kama wanaotafuta hifadhi, ikiwaona kwa wingi kama wahamiaji wa kiuchumi, na inasema haina wajibu wa kisheria kuwahifadhi.
Nchi imejaribu mbinu mbalimbali za kuwalazimisha watoke nje, ikiwa ni pamoja na kuwapeleka katika gereza la mbali, kushikilia sehemu ya mishahara yao hadi pale watakapokubali kuondoka nchini au kutoa malipo ya fedha taslimu kwa wale wanaokubali kuhamia nchi nyingine yoyote ya Afrika.
Wakosoaji wanaishutumu serikali kwa kujaribu kuwalazimisha wahamiaji hao kuondoka. Chini ya sheria za kimataifa, Israel haiwezi kuwarudisha kwa lazima wahamiaji katika nchi ambayo maisha au uhuru wao unaweza kuwa hatarini.
Netanyahu alisema siku ya Jumapili haoni kuwa kuwafukuza wafuasi wa serikali ya Eritrea lingekuwa tatizo.
Watetezi wa wahamiaji wanasema Israel inapaswa kuwakaribisha wale wanaotafuta hifadhi.
Wapinzani wanadai wahamiaji wameleta uhalifu katika vitongoji vya watu wenye kipato cha chini kusini mwa Tel Aviv ambako wamekaa.
Mapigano hayo yalikuja wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 30 tangu mtawala wa sasa wa Eritrea aingie madarakani, tukio lililofanyika karibu na ubalozi wa Eritrea kusini mwa Tel Aviv.