Picha hii iliyopigwa Mei 5, 2024 mjini Jerusalem yenye ujumbe unaosomeka kupitia kituo cha televisheni cha Al Jazeera ukisema: Matangazo ya Al Jazeera yamesitishwa Israel, kulingana na maelekezo ya serikali. / Picha: AFP  

“Wachunguzi wetu, wakisaidiwa na polisi, walivamia ofisi za Al Jazeera mjini nakukusanya vifaa vyote,” Waziri wa Mawasiliano mwenye mrengo wa kulia, Shlomo Karhi alisema kupitia ukurasa wake wa X.

Katika taarifa yake ya Jumapili, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu aliweka wazi nia ya nchi yake kukifunga kituo hicho.

Mwezi ulipota, bunge la nchi hiyo, maarufu kama Knesset, lilipitisha muswada wa kuruhusu kufungwa kwa kituo cha Televisheni cha Al Jazeera.

Sheria hiyo inampa waziri wa mawasiliano, mamlaka ya kuzima mitandao ya kigeni inayofanya kazi nchini Israel na kunyang'anya vifaa vyao ikiwa waziri wa ulinzi atabainisha kuwa matangazo yao yanaleta "athari kwa usalama wa taifa."

Kitendo cha Jinai

Televisheni hiyo yenye makao yake makuu mjini Doha ilishutumu uamuzi wa serikali ya Israeli wa kufunga ofisi zake kama "kitendo cha uhalifu."

“Cha ajabu wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani; serikali ya Israel imefunga ofisi za Al Jazeera, na kuzuia umma kupata maudhui yake, na kupuuza misingi inayotambulika ulimwenguni ya uhuru wa kujieleza," taarifa hiyo ilisema.

"Al Jazeera inahimiza mashirika yote yanayohusika na uhuru wa vyombo vya habari, haki za binadamu, kulaani mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya waandishi wa habari na vyombo vya habari na Israel, na kuwawajibisha wale waliohusika," iliongeza.

Uamuzi huo umeongeza chuki ya muda mrefu ya Israel dhidi ya Al Jazeera.

Pia imetishia kuzidisha mvutano kati yake na Qatar, ambayo inamiliki chaneli hiyo, wakati ambapo serikali ya Doha ina jukumu kubwa katika juhudi za upatanishi ili kusitisha vita huko Gaza.

Israel imekuwa na uhusiano mbaya na Al Jazeera kwa muda mrefu, ikiishutumu kwa upendeleo dhidi yake.

Al Jazeera ni mojawapo ya vyombo vichache vya habari vya kimataifa vilivyosalia Gaza wakati wote wa vita, vikitangaza mauaji ya Israel kutokana na matukio ya umwagaji damu ya mashambulizi ya anga na hospitali zilizojaa watu.

TRT Afrika
AP