Gerard Motondi ni mchongaji mkuu ambaye ameunda sanamu nyingi duniani kote. /Picha: Motondi

Na Pauline Odhiambo

Kenya, ikiwa na historia ndefu ya kutoa mabingwa wa Olimpiki katika uwanja wa riadha, ilipata mshindi ambaye hakutarajiwa katika Michezo ya 2008 huko Beijing.

Gerard Motondi, mchongaji sanamu na mwalimu, alishinda Tuzo ya Mwenge wa Olimpiki mwaka huo katika shindano la sanaa nzuri lililoandaliwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki kando ya Michezo hiyo.

Mchongo wa Motondi wenye urefu wa mita mbili, ulionyesha samaki wawili wakiwa wamekumbatiana, wakiashiria maelewano kama ari ya kudumu ya tamasha kuu la michezo, hadi mahakimu walipigwa na butwaa.

Miaka 16 baada ya kuwashinda wasanii wengine 10,000 kwa medali ya dhahabu, Michezo ya Olimpiki ya Paris ya 2024 ilishuhudia jina la Motondi likivuma ghafla kwenye mitandao ya kijamii nchini Kenya.

Sababu? Sanamu tatu zinazodaiwa kuwa mbovu za wasanii wengine kwa heshima ya wanariadha mabingwa nchini.

Mchongaji hodari

Huku wananchi waliokasirishwa na madai ya kuchukiza ya watu wanaojifanya ni wachongaji, wakionyesha hasira zao kwenye mitandao ya kijamii, wengi wao 'walimtag' Motondi mwenye umri wa miaka 59, wakishangaa kwa nini mchongaji stadi kama yeye hakuchaguliwa kwa mradi huo.

"Suali lilijuwa: Je, jambo kama hilo linawezaje kuruhusiwa?" Motondi anaiambia TRT Afrika.

"Lakini basi, hakuna mtu kutoka kwa serikali au wizara ya michezo aliyewasiliana na mimi ili kutengeneza sanamu kwa heshima ya wanariadha wetu."

Sanamu hizo tatu zenye utata zilikuwa zimezinduliwa kabla ya hafla ya kutoa hadhi ya jiji kwa mji wa Eldoret, ambapo wanariadha wengi mashuhuri wa Kenya wanatoka.

Wakitaka sanamu hizo ziondolewe, Wakenya wengi walichapisha picha za kulinganisha sanamu zilizoundwa nchini Marekani na mataifa mengine kwa heshima ya wanariadha wa Kenya, na sanamu iliyochongwa mjini Eldoret.

Baada ya sanamu hizo kuangushwa, kulizuka kelele mpya kwa Motondi apewe jukumu la kuchonga sanamu inayolingana na hadhi ya wanariadha wanaotunukiwa.

Maafisa wa serikali waliwasiliana na mchongaji mashuhuri ili aweze kuchonga sanamu inayolingana na hadhi ya wanariadha wakubwa kama hao.

Motondi anaweza kuchonga chuma lakini anapendelea mawe. /Picha: Motondi

Uchongaji wa mawe

Motondi alizaliwa Tabaka huko Kisii, kitovu maarufu cha kuchonga mawe katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki na mojawapo ya viwanda vyake vya kitamaduni vya uchongaji wa kutumia mikono.

Akiwa mtoto, Motondi alijifunza ufundi wa kuchonga mawe ya kwa kutengeneza mifano ya ndege, samaki na wanyama. Anapendela kutumia mawe kuliko zana zingine.

"Mawe ni nyenzo ya asili; haiwezi kuchafua mazingira na inaweza kudumu mamilioni ya miaka," anaelezea.

"Mawe pia haina thamani ya kuuzwa barabarani skrepu, jambo ambalo huiokoa kutokana na kuharibiwa, kama ilivyo kawaida kwa sanamu za chuma katika maeneo ya umma.

Pia, ni sugu kwa mabadiliko ya hali ya hewa na haiwezi kuharibiwa na moto," anaongeza Motondi ambaye alipewa pongezi za rais na aliyekuwa rais wa Kenya Mwai Kibaki mwaka wa 2011.

Katikati ya miaka ya 80, Motondi alikuwa sehemu ya kundi la kwanza la walimu nchini kusaidia kutambulisha sanaa nzuri kwa watoto kama sehemu ya mtaala wa kitaifa. Anabaki kuwa mwalimu mwenye bidii.

Motondi alishinda Tuzo ya Mwenge wa Olimpiki katika mashindano ya sanaa nzuri katika Olimpiki ya Beijing ya 2008. Picha: Motondi

Kubadilisha mienendo

Katika utamaduni wa jadi wa Kisii, wanawake hawakuruhusiwa kuchonga mawe.

Jukumu lao mara nyingi lilikuwa ni kukusanya na kusafirisha mawe. Motondi amedhamiria kubadilisha mienendo ya kitamaduni kwa kuwafunza wanawake kadhaa katika uchongaji na kuhakikisha wameshirikishwa.

"Wanawake wanatengeneza sanamu za kupendeza, na miundo yao inauzwa zaidi ya soko la kawaida la watalii," anaiambia TRT Afrika.

"Uchongaji wa wanawake pia umeongeza kipato cha kaya nyingi."

Mchoro wa Motondi unaoitwa 'Sister Cities' umesimamshwa katika Jiji la Chengdu la Uchina, Mkoa wa Sichuan. /Picha: Motondi

Mnamo 2011, Motondi aliandaa kongamano la kitamaduni lililoitwa "African Stones Talk", ambapo wanawake wa nyumbani wangeweza kuonyesha ujuzi wao na kutoa mafunzo na wataalam wengine katika uwanja huo.

Pia ametoa mafunzo kwa wafanyakazi wa madini kwa "kuchanganya mitazamo ya kitaaluma, kitamaduni na biashara", na kuwa chachu ya kupunguza vifo katika sekta hiyo.

Kupamba miji

Moja ya sanamu za marumaru za Motondi, "On the Marks", zimesimamishwa kwenye Citizen Square Park katika mji wa Shenzhen wa Guangdong nchini China.

Mwingine, kwa jina "Fair Play", avutia macho katika idara ya sanaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Kwa miaka mingi, amechonga takriban kazi za sanaa 25 ulimwenguni kote, zikiwemo za Uturuki, Urusi, Kanada, Marekani, India, Korea Kusini, na UAE.

Huko Uturuki, sanamu ya marumaru ya "New Life" ya Motondi imesimamishwa katika mji mkuu wa Mersin katika eneo la kusini mwa nchi.

Motondi amechonga takriban kazi 25 za sanaa duniani kote zikiwemo za Uturuki na Urusi. Picha: Motondi

Alikuwa sehemu ya timu ya wasanii walioalikwa Dubai kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuunda sanamu za marumaru mwaka wa 2008 katika eneo ambapo jengo refu zaidi duniani - Burj Khalifa - sasa linasimama.

"Katika nchi zote nilizofanya kazi, sanamu huadhimisha historia, utamaduni, na mafanikio ya watu wa maeneo hayo," anasema.

Mnamo 2013, alipokea ruzuku kutoka kwa serikali ya Kenya kuunda sanamu ya Mashujaa katika bustani ya Uhuru, Nairobi, ambapo bendera ya Kenya ilipandishwa kwa mara ya kwanza mnamo 1963 kuashiria uhuru wa taifa hilo kutoka kwa wakoloni.

Miaka miwili baadaye, aliunda mchoro mwingine, "Love for the Natiom," ambao uliwekwa katika eneo hilo hilo.

Kwa sasa Motondi anafanya kazi ya kutengeneza sanamu katika Jiji la Tatu nchini Kenya. /Picha: Motondi

"Mchongo huu unaonyesha upendo na mapambano ya mama, kama vile wapigania uhuru wetu walivyojitolea maisha yao kwa taifa," anaiambia TRT Afrika.

Mnamo 2022, serikali ya Kenya ilizindua sanamu ya wapigania uhuru Dedan Kimathi na Mekatilili wa Menza.

Sanamu zote mbili, zilizotengenezwa kwa graniti ya rangi waridi, zimesimamishwa kwenye Jumba la Makumbusho ya Kitaifa ya Kenya.

"Lengo langu ni kuendelea kuunda sanamu na minara inayoweza kupamba miji kote ulimwenguni," asema Motondi.

"Pia ninatumai kuanzisha chuo ili kuendelea kutoa mafunzo kwa watu wanaopenda uchongaji."

Lengo la Motondi ni kuchonga sanamu zaidi ili kupamba miji kote ulimwenguni. /Picha: Motondi
TRT Afrika