Rais Bola Tinubu wa Nigeria

Jumuiya ya Kikanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS ,imeikosoa uongozi wa mapinduzi wa Niger kwa mpango wao wa kumshtaki Rais aliyepinduliwa Mohamed Bazoum.

Viongozi wa mapinduzi wanamshtaki Bazoum kwa uhaini mkubwa na kuhatarisha usalama wa Niger.

Ikiwa atashtakiwa na kupatikana na hatia, Bazoum anaweza kukabiliwa na adhabu ya kifo, kulingana na Kanuni ya Adhabu ya nchi hiyo.

Jeshi nchini Niger awali lilidai kuwa Bazoum alikuwa ana mawasiliano ya mara kwa mara na viongozi wa kigeni wanaopinga serikali ya mpito na wameweka vikwazo kwa nchi hiyo.

Katika majibu yake, ECOWAS inasema "imegundua kwa mshangao jaribio la kumshitaki Mohamed Bazoum kwa mashtaka ya uhaini mkubwa."

Uchochezi

ECOWAS imeongeza kuwa "inalaani hatua hii kwa sababu inawakilisha aina nyingine ya kichochezi na inapingana na nia iliyoripotiwa ya mamlaka ya kijeshi katika Jamhuri ya Niger ya kurejesha utaratibu wa kikatiba kwa njia ya amani."

Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, jumuiya hiyo ya kikanda ya Afrika Magharibi ilisisitiza kuwa Bazoum "bado ni Rais aliyechaguliwa kidemokrasia wa Jamhuri ya Niger anayetambuliwa na ECOWAS na jumuiya ya kimataifa."

"ECOWAS inalaani kuzuiliwa kwake kinyume cha sheria na inaitaka kutolewa kwake mara moja na kurejeshwa madarakani," ilisema taasisi hiyo ya kikanda.

Kulingana na kiongozi aliyetangaza mwenyewe wa Jamhuri ya Niger, Abdourahamane Tchiani, mapinduzi dhidi ya Bazoum mnamo Julai 26 yalikuwa na nia njema, na kwamba yalifanyika kuzuia kusambaratika kwa nchi.

Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi, Kanali Mkuu Amadou Abdramane, kuna ushahidi wa kutosha kumshtaki Bazoum kwa uhaini mkubwa.

Hata hivyo, wanajeshi wanasema wako tayari kukutana na maafisa wa ECOWAS ili kupata suluhisho la amani kwa mzozo wa uongozi nchini Niger.

Pamoja na vikwazo, ECOWAS imeanzisha kikosi chake cha dharura kwa jitihada za kurejesha Bazoum madarakani.

TRT Afrika