Siku ya Oktoba 29, 2024 raia wa Hispania walikumbwa na mafuriko makubwa yaliogharimu maisha ya zaidi ya watu 220 na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu.
Haya hayakuwa mafuriko ya kwanza kutokea barani Ulaya, na wala hayatokuwa ya mwisho huku janga la kuongezeka joto ulimwenguni likishika kasi.
Sayari yetu inaendelea kushuhudia mabadiliko ya mara kwa mara ya tabia nchi, yanayovuka viwango vya kawaida vilivyobashiriwa na wanasayansi na watafiti wengine. Ripoti zinaonesha kuwa, mabadiliko hayo yamevuka kiwango cha nyuzi joto 1.5, ukilinganisha na miaka ya kuanzia 1850 hadi 1900.
Mabadiliko haya yanaashiria janga kubwa mbele yetu, kama vile kuongezeka kwa vina vya bahari na upotevu wa baionwai.
Ripoti iliyotolewa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ilionesha kuwa uzalishaji wa hewa chafu ulifikia viwango vya juu mwaka 2023, ikiashiria nyakati mbaya kwa miaka ijayo.
Hewa ya Kaboni, ndio kinara wa uchafuzi huo, ikiongezeka kwa asilimia zaidi ya 10 ndani ya miongo miwili tu.
Wanasayansi wanabashiri kuwa mwaka 2024 utakuwa wenye joto kali zaidi. Kulingana na watafiti, Julai 222, 2024 ilikuwa ndio siku yenye joto zaidi ulimwenguni, huku viwango vya joto vikifikia nyuzi joto 17.15.
Kupanda kwa wastani wa halijoto ni kiashiria kibaya, chenye kuonesha hali mbaya ya hewa.
Watu ndio wanaoendelea kulipa gharama za mabadiliko haya, huku nchi zinazoendelea zikibeba mzigo mkubwa. Hivi karibuni, utafiti uliofanywa na Chuo cha Imperial London, unaonesha kuwa mabadiliko ya tabia nchi yamesababisha vifo 570,000 toka mwaka 2004, huku ukame wa mwaka 2011 nchini Somalia ukigharimu maisha ya watu 258,000.
Nchi zinazopotea
Wanasayansi wanakubali kuwa kuendelea kwa shughuli za viwandani na utoaji wa gesi usiodhibitiwa kutasababisha ongezeko la joto duniani la nyuzi 2.7 kufikia mwisho wa karne hii. Hali hii itasababisha kuzamishwa kwa nchi na visiwa kama vile Bangladesh, Maldives, na Alexandria, jiji la pwani la Misri, kutokana na kuongezeka kwa viwango vya bahari. Pia litatishia usalama wa chakula, kuvuruga mifumo ya ikolojia, na kudhoofisha uchumi wa kimataifa.
Kwa bahati mbaya, binadamu wanahusika na majanga haya kutokana na matumizi mabaya ya rasilimali za mazingira na ongezeko la shughuli za kibinadamu.
Hali hii mbaya ilimlazimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuonya mara kadhaa kuwa dunia yetu inaelekea ‘mahala pabaya zaidi’.
Amehimiza mabadiliko ya haraka kwa uchumi wa kijana, akisisitiza haja ya ushirikiano zaidi kati ya nchi zilizoendelea na zinazoinukia kiuchumi, akizingatia kuharakisha mabadiliko kutoka kwa nishati ya mafuta. Zaidi ya hayo, pia alitoa wito wa usaidizi wa kutosha wa kifedha ili kusaidia mataifa maskini kupunguza uzalishaji na kukabiliana na athari zinazoweza kuepukika za ongezeko la joto duniani.
Sera na Ahadi
Licha ya ahadi za nchi kwenye Mkataba wa Paris unaolenga kutenga kiwango cha joto kuwa chini ya 1.5 ili kuepusha athari mbaya zaidi za mabadiliko ya hali ya hewa, pengo kati ya ahadi na sera halisi linaendelea kupanuka mwaka baada ya mwaka. Majibu ya kimataifa mara nyingi huonekana kuwa ya kukatisha tamaa na kutotosheleza kushughulikia ukubwa wa changamoto.
Sera hizi sio tu zisizo za haki bali pia zinaweka rehani maisha ya mamilioni, hasa katika maeneo hatarishi kama vile Afrika na maeneo mengine.
Suluhisho lenye matumaini
Bado kuna matumaini ya kuepuka athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabia nchi. Umoja wa Mataifa unasema kuwa teknolojia za sasa zinaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa utoaji wa hewa chafu ifikapo mwaka 2030 na 2035. Wataalamu wanasisitiza kwamba uzalishaji wa kaboni duniani lazima upungue asilimia 45 ifikapo 2030 na hata kufikia sifuri ifikapo 2050.
Hatua muhimu ni pamoja na kutekeleza Mipango ya Kitaifa, kupunguza matumizi ya mafuta kwa asilimia 30 ifikapo 2030, kumaliza makaa ya mawe ifikapo 2040, na kuhakikisha mataifa tajiri yanatoa ufadhili unaohitajika.
Kufikia malengo haya kunahitaji kujitolea kwa nguvu kutoka kwa watu binafsi, serikali, na mashirika mbalimbali.
Tatizo la mabadiliko ya tabia nchi halihusiani na mazingira tu bali maisha ya binadamu kwa ujumla. Maafa tunayoshuhudia leo yanapaswa kuwa tahadhari kwetu, kuchukua hatua za haraka. Swali sasa ni: Je, tuko tayari kubeba jukumu hili, au tutasalia kuwa watazamaji tu wakati sayari yetu inapoelekea hatua ya kutorudi tena?
Yasmine Bouldjedri ni mwandishi kutoka Algeria mwenye uzoefu wa miaka 15.