Chama tawala nchini Tanzania Jumapili kimemteua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wake katika uchaguzi wa urais unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Hassan aliingia madarakani mwaka 2021 baada ya kifo cha ghafla cha mtangulizi wake John Magufuli.
Chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilifanya mkutano mkuu mwishoni mwa wiki mwishoni mwa wiki ambapo kilisema kimemtaja kuwa mgombea pekee katika uchaguzi wa Oktoba.
Naye Rais Samia punde baad aya kutangazwa kugombea Urais, alimteua Katiu Mkuu wa CCM Dkt Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea wake mwenza katika kinyanganyiro hicho.
''Daktari Nchimbi ataendelea kuwa Katibu Mkuu wa chama, hadi uchaguzi utakapofanyika,'' alisema Rais Samia.
Baada ya kushika madaraka, Hassan alisifiwa awali kwa kulegeza vikwazo ambavyo mtangulizi wake Magufuli aliviwekea upinzani na vyombo vya habari nchini yenye takriban watu milioni 67.
Lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu na serikali za Magharibi yamekosoa kile wanachokiona kuwa ni ukandamizaji upya, kukamatwa kwa wanasiasa wa chama cha CHADEMA pamoja na kutekwa na mauaji ya viongozi wa upinzani.
Dkt Philip Mpango aomba kupumzika
Katika tangazo lingine lililowaacha wengi midomo wazi, Rais Samia alitangaza kujiuzulu kwa Dkta Philip Mpango kutoka wadhifa wake kama Makamu wa Rais.
Rais Samia alisema, Dkt Mpango alimwandikia barua kutaka kujiuzulu ili akapumzike.
''Anasema yeye sasa ana miaka 68 na angependa kuishi zaidi kwa hiyo naomba nipumzisheni, nikambishia bishia wiki iliyopita, lakini hapa akanikabidhi barua yangu hii, sikumjibu, lakini nilipoenda kwa kamati kuu nikawaeleza hiyo halina kwa pamoja wote tukakubali tumpumzishe,'' aliongeza Dkt Samia.
Hakuna sababu rasmi zilizotolewa za Dkt Mpango kutaka kujiondoa kutoka wadhifa huo, ila Rais Samia alitaja kuwa hazikuwa sababu za kazi.
Dkt Mpango aliwahi kudokezwa kuwa angewania nafasi ya Makamu wa kwanza mwenyekiti wa Tanzania Bara, japo mwenyewe alipuuza madai hayo katika hotuba yake kwa Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa CCM uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dodoma.
Haijabainika wazi iwapo Dkt Mpango atajiondoa kabisa kutoka siasa baada ya kuachia nafasi hiyo ya Makamu wa Rais.