Vikosi vya usalama vikiwa katika mitaa ya mji wa Dakar tayari kukabiliana na waandamanaji wanaopinga kuahirishwa kwa uchaguzi wa Februari 25. Photo: Reuters Archive

Baraza la Katiba nchini Senegal limesema uamuzi wa bunge wa kuahirisha uchaguzi wa urais wa Februari 25 haukufuata katiba.

Wagombea wa upinzani na wabunge wamewasilisha pingamizi kadhaa kuhusiana na mswada wa bunge wa wiki iliyopita, ambao pia umeongeza muda wa Rais Macky Sall ambao wakosoaji wanasema umeleta 'mapinduzi ya kikatiba.'

Baraza la Katiba nchini Senegal siku ya Alhamisi limefuta tangazo lililosainiwa na Rais Macky Sall la kuahirisha uchaguzi, hayo ni kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na majaji saba wa mahakama hiyo.

Tangazo la kuahirishwa, wiki chache tu kabla ya tarehe ya uchaguzi ya Februari, 25, limesababisha vurugu kuibuka nchini humo kati wa waandamanaji na vikosi vya ulinzi mjini Dakari na maeneo mengine ya nje ya mji.

Vurugu zimeshuhudiwa nchini Senegal baada ya waandamanaji kuingia barabarani kupinga uamuzi wa kuahirisha uchaguzi. 

Jumuia ya Kanda ya Afrika Magharibi ECOWAS na mataifa mengine ya kigeni yenye nguvu yamemtaka Sall kuirudisha nchi katika utaratibu wa kawaida wa uchaguzi.

Watu watatu wameuawa katika maandamano ya kupinga kuahirishwa kwa uchaguzi, huku kukiwa na wasiwasi kwamba, nchi iliyobaki katika utawala wa kidemokrasia katika eneo la Afrika Magharibi iko hatarini.

TRT Afrika