Bassirou Diomaye Faye ameshinda uchaguzi wa rais wa Senegal, matokeo ya awali yanaonyesha, lakini Faye ni nani, na amefikaje hapa, kutoka jela hadi urais | Picha: Reuters

Waziri mkuu wa zamani wa Senegal amekubali kushindwa katika uchaguzi wa urais kwa mgombea wa upinzani kutokana na matokeo ya awali siku moja baada ya kura kupigwa nchini humo.

Amadou Ba katika taarifa iliyoshirikiwa na kampeni yake siku ya Jumatatu alisema anampongeza mgombea wa upinzani Bassirou Diomaye Diakhar Faye na kumtakia mafanikio.

Ushindi wa duru ya kwanza ulionyesha kufadhaika kwa vijana walio na ukosefu mkubwa wa ajira na wasiwasi juu ya utawala katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Faye, akiungwa mkono na kiongozi maarufu wa upinzani Ousmane Sonko, ameapa kuilinda Senegal dhidi ya ufisadi wa serikali.

Faye ni nani?

Akiwa na umri wa miaka 44, Bassirou Diomaye Faye amekuwa rais mwenye umri mdogo zaidi wa Senegal.

Amezaliwa Machi 25, 1980, katika jamii ndogo ya Ndiaganiao katika jimbo la Thiès. Ana shahada ya uzamivu katika sheria, na pia amesomea shahada yake ya kwanza katika Chuo cha Taifa cha Utumishi wa Umma.

Amejiunga na Kurugenzi Kuu ya Taifa ya Kodi na Majengo mwaka 2007.

Bassirou Diomaye Diakhar Faye atahudumu kama rais wa tano wa Senegal. / Picha: Getty

Ni mwanzilishi wa Chama cha African Patriots of Senegal for Work, Ethics and Fraternity (Pastef), kilichoundwa mwaka 2014.

Aprili 14, 2023 alikamatwa na kushtakiwa kwa ‘kuhatarisha usalama wa umma’ baada ya kupinga matumizi ya mfumo wa sheria dhidi ya mwake Ousmane Sonko.

Kwa sababu kesi yake haikutolewa hukumu, ameweza kusimama kama mgombea urais, tofauti na Sonko.

Diomaye Faye, ambae hakuwa anajulikana na wengi mpaka mwaka mmoja uliopita, alipata umaarufu wake baada ya chama chao cha Pastef kushambuliwa, lakini zaidi kupitishwa kwa kiongozi wao Ousmane Sonko. 7

Wanasiasa wote walinufaika na sheria ya msamaha hivyo kuachiwa siku 10 kabla ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa, ushindi wa Diomaye Faye na chama chake, umeleta tafakuri na msisimko wa hali ya juu.

Anajiona mwenyewe kama mgombea atakaeleta mabadiliko ya kimfumo na mwana Afrika.

Mpango wake unatilia mkazo kurudishwa kwa ‘mamlaka ya taifa,’ ambayo anadai imeuzwa kwa wageni.

Ameahidi kupambana na ufisadi na kugawa mali kwa usawa zaidi, na pia ameahidi kujadili upya mikataba ya madini, gesi na mafuta, katika nchi ambayo inaweza kuanza kuzalisha gesi na mafuta kufikia mwisho wa mwaka huu.

Uchaguzi huu umeangaliwa kwa karibu kufuatia miaka mitatu ya vurugu katika nchi ambayo ni miongoni mwa nchi zenye utulivu mkubwa barani.

Kimkakati, Senegal inaendelea kuwa na uhusiano mzuri na nchi za Magharibi katika wakati ambapo Urusi imekuwa ikidumisha nafasi yake katika kanda hiyo.

TRT Afrika