Zaidi ya watu 50, wakiwemo wanawake na watoto, waliuawa katika mashambulizi kwenye mpaka wa Sudan Kusini na Sudan, afisa wa eneo hilo alisema Jumatatu, katika tukio baya zaidi katika mfululizo wa mashambulizi tangu 2021 yanayohusiana na mzozo wa mpaka.
Vijana wenye silaha kutoka Jimbo la Warrap nchini Sudan Kusini walifanya uvamizi katika eneo jirani la Abyei, alisema Bulis Koch, waziri wa habari wa Abyei.
Abyei ni eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta ambalo linasimamiwa kwa pamoja na Sudan Kusini na Sudan, ambazo zote zina madai yake.
''Watu 52, miongoni mwao wanawake, watoto na maafisa wa polisi, waliuawa wakati wa mashambulizi ya Jumamosi. Watu wengine 64 walijeruhiwa,'' Koch aliambia Reuters.
"Kwa sababu ya hali mbaya ya usalama iliyopo, ambayo imezua hofu na wasiwasi, tumeweka amri ya kutotoka nje," alisema.
Mamia wakimbia makazi yao
Mlinda amani wa Ghana kutoka kikosi cha Umoja wa Mataifa kilichopo Abyei aliuawa wakati kituo chake katika mji wa Agok kiliposhambuliwa wakati wa ghasia hizo, Kikosi cha Usalama cha Muda cha Umoja wa Mataifa cha Abyei (UNISFA) kilisema Jumapili.
Koch alisema mamia ya raia waliokimbia makazi yao wametafuta hifadhi katika kambi ya UNISFA.
William Wol, waziri wa habari wa Jimbo la Warrap, alisema serikali yake itafanya uchunguzi wa pamoja na utawala wa Abyei.
Kumekuwa na mapigano ya mara kwa mara huko Abyei kati ya makundi hasimu ya kabila la Dinka kuhusiana na eneo la mpaka wa kiutawala ambalo ni chanzo cha mapato makubwa ya kodi.
Koch alisema vijana wa Dinka kutoka Warrap na vikosi vya kiongozi wa waasi kutoka kabila la Nuer walifanya mashambulizi dhidi ya Dinkas na Nuers huko Abyei.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini, vilivyopiganwa kwa kiasi kikubwa katika misingi ya kikabila kati ya makabila ya Dinka na Nuer, vilisababisha mamia ya maelfu ya vifo kati ya 2013 na 2018.
Tangu wakati huo, mapigano ya mara kwa mara kati ya vikundi vilivyojihami yameendelea kuua na kusababisha wengine wengi kupoteza makao. Mapigano mjini Abyei mwezi Novemba yalisababisha vifo vya takriban watu 32.