Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ametoa wito kwa wanajeshi wa kigeni ambao hawajaalikwa kuondoka DRC.  /Picha: AFP

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema siku ya Jumatatu kwamba kunatakiwa kuanzishwa mchakato wa kuondolewa kwa "majeshi ya kigeni ambayo hayajaalikwa" kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

"Tuna jukumu la kuunga mkono juhudi zote za kuleta amani na utulivu kwa moja ya taifa la Afrika, ambalo limekumbwa na vita kwa zaidi ya miongo mitatu," Ramaphosa alisema katika taarifa yake baada ya mkutano wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika uliofanyika Ijumaa na Jumamosi.

Amesisitiza kuwa nchi kadhaa za EAC, ikiwa ni pamoja na Uganda, Burundi, Tanzania na Rwanda, zina mipaka ya pamoja na Congo na "zimeathiriwa moja kwa moja" na kuongezeka kwa mashariki mwa nchi hiyo. Mkutano huo wa pamoja "umethibitisha uhuru, na mamlaka ya eneo la DRC," alisema Ramaphosa.

"Hii ina maana kwamba mchakato lazima uandaliwe kwa wanajeshi wa kigeni ambao hawajaalikwa kuondoka DRC."

Wakati Ramaphosa hakutaja nchi yoyote mahsusi, DRC ililaumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 na kuishutumu nchi hiyo kwa kutuma vikosi vyake mashariki mwa Congo wakati mashambulizi ya hivi punde yalipoanza.

Rwanda imekanusha mara kwa mara madai ya kuwaunga mkono M23.

Pia alisema kwamba hatua zilizochukuliwa katika mkutano huo "hatimaye zitasababisha kupunguzwa" kwa wanajeshi kutoka ujumbe wa SADC nchini DRC.

Mkutano huo wa kihistoria, ulioandaliwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan jijini Dar es Salaam, mji mkubwa zaidi nchini Tanzania, uliwaleta pamoja wakuu sita wa nchi wanachama wa EAC na SADC yenye wanachama 16.

Wakuu wa majeshi wa jumuiya hizo mbili za Afrika walitakiwa kukutana ndani ya siku tano ili kutoa muelekeo wa kitaalmu wa kutekeleza usitishaji vita na kurejesha amani Goma.

Mkutano wa pamoja wa mawaziri hao utafanyika ndani ya siku 30 ili kutathmini hatua zitakazopendekezwa na wakuu wa majeshi. Waasi wa M23 sasa wanadai udhibiti wa Goma na wametangaza utawala wao wenyewe katika mji huo.

Tangu Januari 26, zaidi ya watu 3,000 wameuawa, 2,880 wamejeruhiwa, na zaidi ya 500,000 wamekimbia makazi yao, na kuongeza idadi ya watu milioni 6.4 ambao tayari wamekimbia makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa.

AA