Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amekaribisha uungwaji mkono wa Washington kwa viti viwili vya kudumu kwa mataifa ya Afrika kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini akasema kuwanyima haki zao za kura ya turufu kutawafanya kuwa "raia wa daraja la pili".
Siku ya Alhamisi, Marekani ilisema inaunga mkono kuunda viti viwili vya kudumu kwa Afrika lakini hawapaswi kutumia kura ya turufu juu ya maazimio ya baraza, tofauti na wanachama wa kudumu wa sasa - Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Marekani.
Kutokuwa na bara la watu bilioni 1.3 wanaowakilishwa kwenye Baraza la Usalama kunapunguza jukumu la Umoja wa Mataifa, Ramaphosa alisema katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa.
Hata hivyo, kuwanyima haki sawa na wanachama wengine wa kudumu "inamaanisha kuwa tunakuwa raia wa daraja la pili kwa mara nyingine tena", alisema.
'Ushiriki wa dhati'
"Tunadai na kuhitaji kwamba tunapaswa kushiriki kikamilifu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa," Ramaphosa alisema.
"Hatuwezi kuwa na ushiriki wa daraja la pili kama Afrika kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa."
Uamuzi kuhusu mataifa yatakayoshikilia viti hivyo viwili utahitaji kuwa juu ya Umoja wa Afrika, aliongeza.
Nafasi ya mzunguko kwa wote
Rais Pual Kagame wa Rwanda amepongeza pendekezo hilo kwa Afrika kupewa uanachama wa kudumu na kwa mtazamo wake ameona afadhali kila nchi ipate fursa ya kushikilia kiti hicho kwa mzunguko.
''Kiti kimoja cha kudumu kingepaswa kushikiliwa na Kamisheni ya AU na kiti cha 2 kishikiliwe na nchi ya Afrika kwa mzunguko!!! Isitolewe kwa nchi moja pekee!'' amesema kagame katika ukurasa wake wa X.
Hata hivyo baadhi ya wanadiplomasia wametahadharisha kutumiwa nafasi hii kuwadhalilisha Waafrika.
Balozi wa zamani wa Kenya katika Umoja wa Mataifa Martin Kimani, amesema kuwa Afrika lazima iwe na mikakati katika kuzingatia mialiko hii ya kirejareja kwa viti vya kudumu vya Baraza la Usalama.
''Bila mageuzi sahihi katika Umoja wa Afrika ofa ya Marekani - ingawa inakaribishwa - inaweza kugeuza Muungano kuwa klabu ya majitu mawili yenye nguvu na wafuasi 53 wanyonge, ikizidisha migawanyiko na kugawanya nia yetu ya pamoja,'' amesma balozi Kimani.
Balozi Kimani aliongeza kuwa mabadiliko kama haya katika Umoja wa Mataifa lazima yaambatane na, kujazilia safari ya kihistoria ya Afrika ya ushirikiano, au yatakuwa hatua za kujizubaisha tu ambazo zinashikilia miundo ya sasa ya mamlaka bila kulinda vyema amani ya kimataifa, usalama, na uhuru wa Afrika.
Mataifa ya Afrika tayari yana viti vitatu visivyo vya kudumu kwenye Baraza la Usalama, vilivyotengwa kwa mzunguko kwa mihula ya miaka miwili.
Mabadiliko yoyote ya uanachama yangehitaji kwanza kupitishwa na kuidhinishwa na theluthi mbili ya nchi wanachama 193.
Mageuzi ya Baraza la Usalama, ambayo yamekwama kwa muda mrefu kwa sababu ya tofauti kati ya wanachama wake wa kudumu, yatahitaji pia kupitishwa kwa kauli moja kati ya mataifa matano ya ngazi ya juu, ambayo yote yana silaha za nyuklia.